Home » , , , » HIVI NDIVYO DENTI ALIVYOTESEKA ICU KWA MIEZI MITANO...INASIKITISHA MNO.......

HIVI NDIVYO DENTI ALIVYOTESEKA ICU KWA MIEZI MITANO...INASIKITISHA MNO.......

Stori: Makongoro Oging’ na Haruni Sanchawa
MATESO ya mwanafunzi Norat Rashid (16), anayesoma kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Mtoni Relini, Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam ni ya kuhuzunisha na kutia huruma kutokana na ajali ya pikipiki aliyoipata miezi nane iliyopita wakati akienda shuleni.

Mwanafunzi Norat Rashid akipatiwa matibabu katika Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) iliyopo Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Norat alimuambia mwandishi wetu hivi karibuni katika Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) katika Hospitali ya Muhimbili Jengo la Mwaisela chumba namba mbili kuwa ajali hiyo aliipata maeneo ya Mtoni kwa Azizi Ally saa za asubuhi wakati akivuka barabara akienda shule.
Alisema mara baada ya ajali alipoteza fahamu na alipozinduka alijikuta amezungukwa na madaktari wa Muhimbili. Katika mahojiano hayo, Norat alikuwa na haya ya kusema:
“Najua huu ndiyo mwisho wangu wa kusoma, ndoto ya kufika chuo kikuu imezimika ghafla kama taa, sikutegemea kama leo hii ningekuwa hivi, nilizaliwa nikiwa sina matatizo, nilikuwa natembea kwenda shule leo hii siinuki, nalishwa kama mtoto mdogo,“Mama ndiye ananiogesha, kila kitu juu yake wakati hana kazi ya kufanya, namuhurumia sana, bora baba angekuwa hai wangesaidiana kunitunza, pole mama…” 

 Muonekano wa jeraha la mguu baada ya kupata ajali ya pikipiki.
ICU MIEZI MITANO
“Ajali niliyopata ilikuwa mbaya sana, sikutegemea kama leo hii ningekuwa hai, kinachoniuma ni kuona niko kitandani siinuki wala kukaa, nimevunjika mguu, kiuno na mbavu napata maumivu kupita kiasi, nipo hapa wodini lakini ni baada ya kukaa katika chumba maalum cha wagonjwa mahututi (ICU) ambao wako chini ya uangalizi wa madaktari kwa miezi mitano.
“Najua muda si mrefu nitaruhusiwa na madaktari kwenda nyumbani, naamini nitakufa, sitachukuwa muda mrefu kutokana na umaskini wetu, mahitaji muhimu sitayapata kwa vile mama hana kazi, tutakula nini, nitavaaje, nitapataje dawa na tutaishi wapi, nyumba yenyewe ni ya kupanga na kodi imeisha, tutaelekea wapi sisi jamani!
“Wakati nikiwa mzima mama alikuwa akizidiwa na majukuma na sasa nimekuwa mlemavu wa kitandani tena wa kutazamwa muda wote! “Bora ningebakia Muhimbili kuliko kumhangaisha mama, sijui kodi ya chumba atapata wapi kwani kabla sijaugua alikuwa akihangaika kufanya biashara ndogondogo na kupata fedha ya matumizi.”

Norat Rashid akiwa katika jengo la Mwaisela chumba namba mbili katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
WALIMU, WANAFUNZI WENZAKE WAMSUSA
“Nikiwa shule wanafunzi wenzangu walikuwa wakinipenda sana, nikiwa Muhimbili walikuja mara moja tu kuniona nilivyoumia, mpaka leo sijawaona. Walimu nao walikuja mara moja kwa sasa hawaonekani, anayenitembelea ni mama peke yake, hata mjomba naye haji sijui kwa nini, au wananiona kama mzigo kwao?
“Kuna wagonjwa wanatembelewa na ndugu zao kuwafariji wakati mwingine kuwaletea chakula lakini kwa upande wangu hakuna wa kunijulia hali, lakini siyo tatizo kubwa kwangu, yote namwachia Mungu.
“Nawaombeni wananchi mlio na moyo wa huruma mnisaidie, mniombee niweze kutembea, nirudi shule nisome kama wenzangu,” alisema Norat huku akitokwa na machozi.
Kwa kuwa Norat hana simu, watakaopenda kumsaidia  wakawaone maofisa wa ustawi wa jamii Muhimbili watawaunganisha naye.

TOA MAONI YAKO HAPA

 
Support : Copyright © 2011. HABARILINE - All Rights Reserved