Home » » Wanafunzi Ilboru wapo kwenye mgomo

Wanafunzi Ilboru wapo kwenye mgomo

  Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi,Phillipo Mulugo.
Mgomo wa wanafunzi wa Sekondari ya Ilboru, iliyopo wilayani Arumeru, kutoingia madarasani uliingia siku ya pili jana, wakishinikiza mwanafunzi mwenzao Ibrahim Kaebo wa kidato cha tatu ‘C’ aliyefukuzwa na bodi bila kupewa nafasi ya kujitetea, kurejeshwa shuleni.
Akizungumza katika ofisi za NIPASHE mjini hapa, alisema yeye ni Makamu Mwenyekiti wa chakula na bwalo, hivyo akiwa kiongozi alikuwa anakabiliwa na changamoto za chakula kuwa kibovu na wenzake kugoma kula, hivyo kama wajibu wake aliandika taarifa, jambo lililomponza kuwa anajifanya mjuaji.

Alisema alimsindikiza mwanafunzi mwenzao hospitalini, (hakumtaja jina), baada ya kuumizwa mkono kwa kuchapwa viboko na mwalimu, jambo lililopelekwa katika bodi kuwa alitaka mwalimu afukuzwe kazi.

Makosa mengine aliyataja kuwa ni kuondoka shuleni bila ruhusa, kutofanya mitihani, kudharau walimu, kuwapiga wanafunzi na kuwajeruhi, kukataa kumeza dawa, jambo ambalo alieleza kuwa siyo la kweli.

Kaebo alisema kinachomsikitisha zaidi ni kumfukuza shuleni hapo bila kumpa nafasi ya kujitetea na kwamba hajawahi kufanya kosa lolote lililosababisha apewe barua ya onyo.

Alisema baada ya kutaka apewe barua yenye kueleza makosa aliyofanya hakupewa, badala yake alipata vitisho vya kutakiwa kuondoka shuleni hapo.

“Nikiwa shuleni Mwalimu Mkuu wetu, Julius Shulla, aliita wanafunzi wenzangu mstarini na kuanza kuwaeleza sababu za kunifukuza, jambo lililowashangaza na kuamua kugoma kuingia madarasani,” alisema.
Kaebo alisema wanafunzi wanagomea mambo mengi ikiwamo tabia ya kubadilishiwa mabweni na walimu bila kuhusisha uongozi wa shule kama mtaala unavyosema.

Kasoro nyingine ni kubadilishiwa ratiba ya chakula na kulazimishwa kuchagua vyakula vya bei nafuu.

Mmoja wa viongozi wa wanafunzi shuleni hapo, ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema alichotendewa mwanafunzi mwenzao siyo haki na makosa hayo siyo ya kweli, maana alikuwa mtetezi wao kama kiongozi.

Alisema hata kama alikosa shule ingempa nafasi ya kujieleza, jambo ambalo hawakubaliani nalo na wataendelea kugoma.

Wanafunzi hao wamegoma kwa kujikusanya kwenye mabweni, bila kuingia madarasani.

Waandishi walikwenda shuleni hapo kutaka kumwona Mkuu wa shule lakini alikataa kuonana nao kwa kile kilichoelezwa kwamba akihitaji kuongea na waandishi atawaita.

CHANZO: NIPASHE

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU YA FACEBOOK HAPA CHINI

TOA MAONI YAKO HAPA

 
Support : Copyright © 2011. HABARILINE - All Rights Reserved