Dar es Salaam. Mtoto Kudra aliyekuwa ameunganika na kiwiliwili cha pacha
mwenza, anaendelea vizuri na matibabu katika Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili (MNH).
Mtoto huyo alifanyiwa upasuaji Alhamisi iliyopita katika Taasisi ya
Mifupa ya Muhimbili (Moi) na kulazwa katika wodi ya wagonjwa wanaohitaji
uangalizi maalumu (ICU), lakini mwishoni mwa wiki iliyopita alitolewa
katika wodi hiyo.
Mama mzazi wa mtoto huyo, Pili Hija, alisema hivi sasa Kudra ananyonya
vizuri na kwamba amekuwa akitaka kufanya hivyo kila wakati
.
“Kwa kweli kudra za Mwenyezi Mungu ndizo zimemweka hai mpaka leo hii,
nilikuwa nimeshakata tamaa kuwa nampoteza mwanangu, nazidi kumuomba
Mungu amwekee mkono wake apone kabisa,” alisema Hija.
Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto katika Hospitali ya Muhimbili, Dk
Zaitun Bokhary, alisema mtoto huyo anaendelea vizuri na mwishoni mwa
mwezi huu atafanyiwa upasuaji mwingine.
“Tunamwacha achangamke kwanza, mwishoni mwa mwezi huu tutamfanyia
upasuaji mwingine wa kumwekea njia ya muda ya kutolewa haja kubwa, kwa
kumpasua ubavuni baada ya hapo ataruhusiwa kwenda nyumbani,” alisema Dk
Bokhary.
Kudra alipewa jina hilo Alhamisi usiku, saa kadhaa baada ya upasuaji
kufanyika chini ya jopo la madaktari saba, walioongozwa na Dk Hamis
Shaaban, mtaalamu wa Ubongo na Uti wa Mgongo kutoka Moi.
Alizaliwa Agosti 18, baada ya mwanamke huyo kujifungulia nyumbani watoto
pacha, huku mmoja akiwa hajakamilika viungo vyote. Pia, kiwiliwili
kilichoungana hakikuwa na kichwa, macho, maini, figo ila alikuwa na
mshipa mmoja wa fahamu ambao ulikuwa umeshikana na mwenzake na
kulazimisha madaktari hao kumfanyia upasuaji.
Mwananchi