Mahojiano baina ya Jeshi la Polisi na Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima yaliyokuwa yanatarajiwa kuendelea jana, ikiwa ni siku mbili baada ya kuachiwa kwa dhamana na jeshi hilo, jana yalikwama kuendelea kutokana na kile kilichoelezwa kutoimarika kwa afya ya askofu huyo, na sasa yatafanyika Alhamisi ijayo.
Gwajima
alidaiwa kuzimia wakati akihojiwa na makachero wa Polisi waliokuwa
wanamhoji, alipojisalimisha alasiri ya Ijumaa iliyopita baada ya
kutakiwa kufanya hivyo, kutokana na kufunguliwa jalada la malalamiko ya
kumkashifu Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam,
Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo.
Kutokana
na hali hiyo iliyotokea majira ya saa tatu usiku wakati akiendelea na
mahojiano yaliyoanzia alasiri, alikimbizwa Hospitali ya TMJ, Mikocheni
akiwa chini ya ulinzi wa Polisi hadi aliporuhusiwa kutoka Jumanne wiki
hii na baadaye kuachiwa kwa dhamana.
Mwanasheria
wa Askofu Gwajima, John Mallya alithibitisha kuahirishwa kwa mahojiano
kati ya mteja wake na Polisi, akisema mapema jana asubuhi aliripoti
Kikuo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam kama alivyotakiwa kuripoti kituoni
hapo kwa ajili ya mahojiano.
Hata
hivyo, alisema hakuweza kuhojiwa kutokana na kile kinachoelezwa kuwa
afya ya mteja wake haijaimarika vizuri na hivyo wamepangiwa kurudi tena
kituoni hapo Aprili 9 mwaka huu, yaani Alhamisi ijayo kwa ajili ya
mahojiano.
“Mteja
wangu alifika kituoni leo (jana) asubuhi kwa ajili ya mahojiano na pia
kuripoti kama ilivyoagizwa siku alipopatiwa dhamana, hata hivyo afya
yake bado haijaimarika na hivyo imewalazimu polisi wampatie muda zaidi
hadi Aprili 9 atakaporudi tena kwa ajili ya mahojiano,” alisema Mallya.
Hata
hivyo, Mallya alisema hali ya afya ya Gwajima imeanza kuimarika na
kadri siku zinavyozidi kwenda, atakuwa na nguvu na ataendelea na kazi
zake kama kawaida.
Mtumishi
huyo alipatiwa dhamana katika Kituo cha Polisi Oysterbay na kutakiwa
kuripoti Kituo Kikuu cha Kati kwa ajili ya mahojiano zaidi na kusubiri
uchunguzi wa kesi yake ukamilike.