KAMATI ya Vijana Wapenda Amani Tanzania (VIWATA) keshokutwa itawasilisha maombi kwa Mwanasheria Mkuu, ya kupinga kesi aliyofunguliwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS).
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu wa kamati hiyo, Said Mwaipopo, alisema wamechukua uamuzi huo baada ya kujiridhisha kuwa kesi hiyo imefunguliwa na wanaharakati hao kwa utashi wa kisiasa zaidi na haitowaletea Watanzania mapinduzi wanayoyataka.
“Sisi vijana wapenda amani na haki, tumeona kesi hii ni uzushi wa wazi au ajenda za kisiasa za kupanda mbegu za chuki kwa Waziri Mkuu na Mwanasheria wa Serikali,” alisema Mwaipopo.
Alisema kauli aliyoitoa Waziri Mkuu bungeni, kwamba watakaokaidi amri ya vyombo vya dola wapigwe, haikuwa na maana mbaya kama ambavyo imechukuliwa na watu wengi, kwani kabla ya hatua ya kupiga, vyombo hivyo vya dola hufuata kwanza utaratibu na kanuni zao walizojiwekea.
“Hii si kwa polisi nchini, vyombo vyote vya dola duniani, haviwezi kukuangalia pale unapotishia usalama wa mwananchi mwingine, lazima uchukuliwe hatua na ikibidi upigwe kwa ajili ya kutuliza amani na kuhakikisha usalama wa eneo husika,” alisisitiza.
Kamati hiyo pia imeelezea kusikitishwa na namna wanaharakati hao, walivyoichukulia vibaya kauli hiyo ya Pinda na kukimbilia mahakamani, wakati siku za nyuma kulitokea matamshi yenye dalili za kuvunja amani na hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa.
Alitaja matukio hao kuwa ni pamoja na baadhi ya wanasiasa kutamka wazi kuwa “nchi haitatawalika, mauaji ya Mwembechai, mauaji ya vikongwe Shinyanga, mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi, vurugu za Mtwara, vurugu za kisiasa na mabomu Arusha na Morogoro na wananchi kumwagiwa tindikali.
“Hivi karibuni kauawa hadi Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza na vurugu za sasa za kidini na tukirejea nyuma kuna wanasiasa walikaririwa wakisema nchi haitotawalika, mbona watu hawa wa haki za binadamu hatuwaoni wakilalamika au kuchukua hatua kama hii…” alihoji.
Mjumbe wa Kamati hiyo, Andrew Mwila alisema kitendo cha wanaharakati hao kumshitaki Pinda, ni kinyume cha Katiba kwa kuwa inabainisha wazi kuwa mbunge yeyote ana kinga na yuko huru kuzungumza bungeni bila kushitakiwa.
“Kule (bungeni) wana taratibu zao, kama kweli mbunge kazungumza mambo mazito, kuna Kamati ya Maadili, anafikishwa huko lakini ana kinga ya kushitakiwa huku nje, na hilo tumeshuhudia kwani wapo wabunge wamezungumza mambo hatari na hawajashitakiwa, hii kesi ni danganya toto kuna mambo mengine nyuma yake,” alisema.
Kwa upande wake, Wakili kutoka kampuni ya Uwakili ya Austin Wilson, Sweetbert Nkubi, alisema kampuni yake inakamilisha utafiti wake juu ya suala hilo, na inatarajiwa kuwasilisha maombi ya kupinga kesi hiyo dhidi ya Pinda, keshokutwa.
“Tunachotaka ni kumuomba Mwanasheria Mkuu awaingize wateja wetu kwenye kesi hii ili watumie fursa hiyo kupinga mashitaka hayo dhidi ya Waziri Mkuu ambayo yamelenga kutaka ufafanuzi wa Katiba juu ya tamko hilo alilolitoa bungeni,” alisema.