BAADHI ya
wadau wa masuala ya jinsia wamependekeza kuwa ili kukabiliana na masuala ya
ushoga na usagaji, Katiba Mpya iruhusu wafungwa kukutana kimwili na wenza wao,
kwani vitendo hivyo chanzo chake ni gerezani hasa kwa vijana wanaokula 'unga'
na kuvuta bangi.
Hayo yalisemwa juzi kwenye
kikao cha maboresho ya Rasimu ya Katiba Mpya, kilichofanyika siku tatu kwenye
Kijiji cha Makaburini kwa kuratibiwa na asasi ya Tanzania Environment Relatives
Organization (TERO) ya mjini Korogwe kwa ufadhili ya Shirika la The Foundation
for Civil Society la jijini Dar es Salaam.
"Mfungwa akubaliwe
kukutana kimwili na mume au mke wake. Kitendo cha kuwakatalia wafungwa kukutana
kimwili na wake au waume zao kunachochea vitendo vya kufanya mapenzi ya jinsia
moja na vijana wengi wameharibikia gerezani na kujikuta vitendo hivyo vinaingia
mitaani" alisema Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kerenge- Makaburini
Mohamed Mdoe.
Mdoe alisema ili kuimarisha
ulinzi na usalama mabalozi wawe viongozi wa Serikali badala ya chama, kwani
kutokana na vitongoji kuwa vikubwa, Mwenyekiti wa Kitongoji hana uwezo wa
kuratibu watu wote walioingia kwenye kitongoji chake, lakini balozi ana uwezo
kutokana na eneo lake kuwa dogo.
Naye Mwalimu Mkuum, Shule ya
Msingi Makumba, Sisili Mhina alisema hakuna sababu ya kuwafunga watu
waliotukanana ama kuiba vitu vidogo vidogo, huku ni kujaza magereza na
kuliongezea Taifa mzigo na kudai suluhu ya watu hao ni kufungwa kifungo cha nje
wakiwa wanaitumikia jamii.
Naye Hamisi Mijuza alisema vyeti
vya kuzaliwa visitolewe kwenye Ofisi ya Mkuu wa wilaya bali kwenye ofisi za
vijiji na kata kwani hao ndio wanaowajua watoto na wazazi wao kwao ni wapi na
kudai wanapokwenda kwa Mkuu wa Wilaya wanapoteza muda mwingi na gharama bila
sababu za msingi.
Naye Mchungaji wa Kanisa la
Anglikana Kata ya Kerenge, Stephen Daffa alisema Serikali kuogopa kukosolewa na
waandishi wa habari katika masuala ya kitaifa ni sawa na kukimbia kivuli chake,
kwani katika nchi zilizoendelea vyombo vya habari ni mhimili wa nne, na
unasaidia Serikali kujua wapi inakwenda vizuri na wapi inakosea.
"Serikali isiingilie vyombo
vya habari kwa vile vinasaidia kuelimisha umma. Lakini hapo hapo vinakosoa na
kuona mambo yanakwenda vizuri, hivyo kujaribu kuvibana ili visifanye kazi zake vizuri
ni kuchelewesha maendeleo ya wananchi," alisema Mchungaji Daffa.