Showing posts with label TANZANIA. Show all posts
Showing posts with label TANZANIA. Show all posts

Upinzani ‘wawasha moto’ Zanzibar,wataka Chikawe ajiuzulu kwa taarifa za uongo...


  • Ni kauli iliyotolewa wakati wa mkutano wa hadhara uliovishirikisha vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi

Waziri wa Sheria na Katiba Mathias Chikawe ametakiwa ajiuzulu kwa kutoa taarifa za uongo kwamba Zanzibar ilishirikishwa kabla ya Muswada wa Mabadiliko ya Katiba kuwasilishwa bungeni na kupitishwa na Bunge Septemba mwaka huu.
Msimamo huo ulitolewa na Waziri wa Sheria na Katiba Zanzibar, Aboubakary Khamis Bakari wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliovishirikishwa vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi uliofanyika Uwanja wa Kibandamaiti mjini Unguja jana.
Aboubakari alisema kwamba Zanzibar ilipokea taarifa ya awali ya mabadiliko kuhusu vifungu vinne vya Muswada wa Mabadiliko ya Katiba na kutakiwa Zanzibar itoe maoni na mapendekezo yake, jambo ambalo alisema lilifanyika kupitia Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Hata hivyo, alisema vifungu vya mabadiliko ghafla viliongezwa kutoka vinne hadi 12 bila ya Zanzibar kupewa nafasi ya kujadili vifungu vinane ambavyo vina umuhimu mkubwa katika kupata katiba bora.
“Waziri nimesoma naye Chuo Kikuu mwaka 1972, Chikawe kwa hili amesema uongo vinginevyo ajiuzulu, hafai,” alisema Aboubakari.
Alisema kabla ya kufanyika Waziri akifuatana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Bunge, William Lukuvi walifika Zanzibar na kutaka wajadili vifungu hivyo kwa siku moja jambo ambalo alipinga kulitekeleza.
“Baada ya kuanza kupiga kelele, wenzetu walikuja Zanzibar wakitaka tujadili mabadiliko ya mswada,nikawaambia siwezi kujadili masilahi ya nchi kijuujuu, huko ni kuiuza nchi, siko tayari kufanya hilo,” alisema.
Aboubakari alisema marekebisho yaliyofanyika katika muswada huo na kutoa nafasi kujadili na kupitisha mabadiliko ya Katiba kwa kutumia wingi wa kura ni sawa na wazimu.
Alisema mabadiliko yoyote ya Katiba yanapaswa kutumia theluthi mbili toka pande mbili za Muungano, utaratibu ambao ndiyo umekuwa ukitumika na nchi mbalimbali zenye mfumo kama wa Tanzania. Mwananchi ilipomtafuta Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe kujibu tuhuma hizo alisema Aboubakari ameudanganya umma mchana kweupe kwa vile yeye na Waziri Lukuvi walifika Zanzibar kupeleka rasimu ya muswada na si kujadili na kupokea mapendekezo papo kwa hapo.
Chikawe alisema kwamba walipokabidhi muswada pia walimtaarifu siku ya kuwasilishwa muswada huo katika kikao cha Bunge na kuwataka kutoa maoni na mapendekezo kwa wakati mwafaka kabla ya kujadiliwa na kamati ya Katiba ya Sheria ya Bunge.
Alisema kwamba nyongeza ya marekebisho ya vifungu vinane yalitokana na mapendekezo ya wabunge katika kamati na michango ya wabunge ndani ya Bunge katika utaratibu unaoruhusiwa kisheria.
“Baada ya kamati ya Bunge kukaa, Mbunge Halima Mdee wa Chadema ndiye aliyependekeza kutumika kwa utaratibu wa wingi wa kura katika kupitisha mabadiliko hayo ya Katiba kama hatua ya theluthi mbili itashindwa kufikia mwafaka,” alisema Chikawe.
-mwananchi

POLISI WATIBUA NDOA YA BINTI WA MIAKA 14 HUKO GONGO LA MBOTO....WAWATIA MAHABUSU MAHARUSI WOTE WAWILI...!!




NDOA iliyokuwa tayari kufungwa na shehe kati ya Hamis Ngaumba (35), mkazi wa Bangulo, Ulongoni, Gongo la Mboto, Dar na binti wa miaka 14 anayetajwa kwa jina moja la Zubeda, imesambaratishwa na polisi wa Kituo cha Polisi cha Sitaki-Shari, Dar kutokana na umri wa bi harusi kuwa mdogo, Amani limeidaka hiyo.
Kizaazaa hicho cha aina yake kilichovuta hisia za wengi kilitokea saa 10:00 jioni, Jumapili iliyopita ambapo Shehe Bakari Mgesa wa Msikiti wa Bangulo alikuwa ameanza kutoa mawaidha ya maandalizi ya kufungisha ndoa hiyo lakini ghafla polisi na mapaparazi waliingia na shughuli kuishia hapo.

ISHU ILIKUWA HIVI
Mapema siku ya tukio, msamaria mwema ambaye hakupendezwa na kitendo hicho alitoa taarifa kwa mapaparazi ambao nao waliwataarifu polisi wa Kituo cha Polisi Sitaki-Shari na kupewa maafande kutoka dawati linaloshughulikia unyanyasaji wa kijinsia na kuambatana nao hadi eneo la tukio.

BREKI YA KWANZA KWA MJUMBE
Kabla ya kufika eneo la tukio, breki ya kwanza ilikuwa ni kwa mjumbe wa eneo hilo Shina Namba 10, Erasto Nyakiege ambaye alikiri kusikia taarifa hizo za mtoto kufungishwa ndoa lakini alizipata muda mfupi kabla polisi na waandishi hao kufika eneo hilo.

MJUMBE AUNGANA NA POLISI, MAPAPARAZI
Mapaparazi, polisi na mjumbe huyo waliambatana hadi kwenye nyumba ambayo ilikuwa na shamrashamra za ndoa hiyo na kumkuta shehe akijiandaa kufungisha huku waalikwa wakiwa wameshakaa mkao wa kula ‘mnuso’ (pilau).

MSHTUKO WATOKEA, WATU WAKIMBIA
Mshtuko mkubwa ulitokea eneo la sherehe baada ya watu kuwaona askari, wengine walikimbia kama wanafukuzwa na simba. Bi harusi yeye alikimbilia chumbani huku bwana harusi akijichanganya katikati ya wageni waalikwa lakini polisi walimweka ‘mtukati’.

SHEHE AWA WA KWANZA KUSIMULIA
Akizungumza baada ya kunaswa, Shehe Bakari alisema ndiyo kwanza alikuwa anajiandaa kwa zoezi la kuwafungisha ndoa wawili hao lakini kama angebaini kuwa mtoto huyo ana miaka isiyokidhi vigezo, asingekubali kwa vile hata dini ya Kiislamu hairuhusu mtoto kuolewa mpaka atimize miaka 18 na kuendelea.

BI HARUSI AWA WA PILI KUWEKA BAYANA
Naye bi harusi, Zubeda ambaye anaishi na bibi yake aitwaye Bibi Abuu, alieleza kuwa ndoa hiyo ilikuwa ni kama utani kwani mwanamme huyo alikuwa akimtania tangu akiwa mdogo akimwambia kuwa akikua atamuoa, hivyo akawa anamuita mchumba lakini hakuwahi hata siku moja kumtongoza.

MAHARI ILIVYOPELEKWA
Zubeda alisema cha kushangaza siku moja aliwaona wazazi wa kijana huyo wakipeleka barua ya posa na mahari na kumkabidhi mjomba na bibi yake kwani baba yake mzazi anaishi Shinyanga na mama anaishi Tabora, tangu akiwa mdogo anaishi na bibi yake huyo.
“Mimi natamani sana kusoma lakini sina uwezo kwani niliishia darasa la tatu baada ya wazazi wangu kushindwa kunisomesha ndipo bibi akaja kunichukua ndiyo maana suala la kuolewa limenitokea tu bila mwenyewe kupenda. Ilikuwa kama utani lakini wakapokea mahari,” alisema Zubeda huku akilia kwa uchungu.

BIBI AZUNGUMZA HUKU AKIWA AMELEWA TILALILA
Bibi Abuu alipoona mambo yameharibika huku akiwa  tilalila alikimbilia ndani kulala ambapo babu wa kufikia wa Zubeda, James alisema ni kweli mjukuu huyo ana miaka 14 na kuongeza kwamba waliopokea mahari ya mtoto huyo kiasi cha shilingi laki tano na nusu (550,000) ni wajomba pamoja na Bibi Abuu lakini yeye hajui chochote kuhusiana na ndoa hiyo.

KIUMENI WADAI MAHARI
Baada ya sekeseke hilo, ndugu wa upande wa mwanamme walikuja juu na kudai mahari yao huku wakitishia kwamba kama hawatarudishiwa basi wakwe hao watapelekwa polisi kwani hata wao hawakujua kama huyo anayeolewa ni mtoto wa miaka 14.

WAPELEKWA POLISI
Hata hivyo, polisi waliwazoa ndani ya difenda bwana harusi, bi harusi na wajomba wawili ambao ndiyo waliopokea mahari na kwenda kuwaweka nyuma ya nondo kusubiri taratibu za kisheria.

KIJIJI CHA UNGA CHAFUMULIWA DAR,POLISI HAWARUHUSIWI KUINGIA,MABILIONEA WA UNGA WAZUIA KITUO CHA POLISI KUJENGWA...


                Mwili ulioshonewa madawa ya kulevya.
JIJI la Dar es Salaam lina mambo mengi lakini moja ambalo linatisha ni kugundulika kwa kijiji cha madawa ya kulevya ambacho kipo kando ya Bahari ya Hindi.
  Kijiji hicho ni Kunduchi, nje kidogo ya jiji na uchunguzi wa gazeti hili umeonesha kuwa, madawa ya kulevya yenye thamani ya mabilioni ya shilingi yamekuwa yakikamatwa katika eneo hilo.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na Uwazi kwa sharti la kutoandikwa majina yao gazetini, walisema matajiri wengi wa ‘unga’ wamekuwa wakitumia eneo hilo kutokana na kile kilichodaiwa kuwa ni salama kwa shughuli hiyo.
Kijiji cha dawa za kulevya kilichopo Kunduchi jijini Dar.
“Hapa Kunduchi ni kando ya bahari, wengi wanatumia majahazi au boti za uvuvi kuingiza mihadarati hiyo. Wanapoleta madawa yao wanaonekana kama wanatoa samaki au mizigo mingine ya kawaida lakini kumbe ni madawa ya kulevya,” alisema kijana mmoja.
Mzee wa siku nyingi wa kijiji hicho alisema anasikitishwa kuona kuwa kitongoji chao kimekuwa makao makuu ya biashara hiyo haramu ya madawa ya kulevya na yanauzwa wakati serikali ipo.
“Kuna wakati tulitaka sana kijengwe kituo cha polisi lakini tukaambiwa kuna matajiri hawataki hilo, hivyo ajenda hiyo ikaisha na wengi tunaamini matajiri kwa kutumia fedha hawaruhusu kituo cha polisi kuwepo eneo hilo ndiyo maana hakijengwi,” alisema mzee huyo na kuongeza kuwa Kituo cha Polisi cha Silver Sands kiko mbali sana.

Dawa za kulevya.
Uchunguzi zaidi umebaini kuwa watuhumiwa wengi wa madawa hayo haramu wanakamatiwa katika kijiji hicho.
Kwa mfano, Fred William Chande na wenzake wanane waliwahi kukamatwa kwa madai ya kuwa na madawa hayo aina ya heroin yenye thamani ya shilingi bilioni 6.4 Februari 21, 2011 na tayari wamefunguliwa kesi namba 1/ 2012 Mahakama Kuu ya Tanzania.
Chanzo kingine cha habari kilidai kuwa hata madawa aina ya Crystal Methamphetamine kilo 150 yenye thamani ya shilingi bilioni 6.8 walizokamatwa nazo Agness Jerald ‘Masogange’ na Melisa Edward nchini Afrika Kusini chimbuko lake ni Kunduchi.
Naye Mwanaidi Ramadhan na wenzake wanane wanadaiwa kukamatwa na madawa aina ya heroin yenye gramu 2,083.3 ambayo thamani yake ni mamilioni ya shilingi, eneo la Mbezi Beach Kata ya Kunduchi, Dar na tayari polisi wamewafungulia kesi mahakama kuu ambapo jalada lao ni namba 10/2012. Walikamatwa Juni 1, 2011.

Naye Ally Murzai Pirbakshy ‘Haji’ na wenzake watatu walikamatwa wakidaiwa kuwa na  madawa aina ya heroin yenye thamani ya mamilioni ya shilingi na uzito wa gramu 3,053.5 Septemba 7, 2011. Nao wamefikishwa mahakama kuu na kufunguliwa kesi namba 10/2012.
Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya Tanzania, Kamishna Godfrey Nzowa alipoulizwa juu ya kijiji hicho alisema polisi wamekuwa wakifanya kazi kubwa  kwa kushirikiana na wananchi na matokeo yake yamekuwa mazuri.
“Yeyote ambaye ana habari juu ya wanaofanya biashara hiyo aje kuniona na njia ya bahari tunaidhibiti, wasijidanyanye kuitumia kwani kuna wenzao walifanya hivyo Lindi tukawakamata, ”alisema Nzowa.

MBARONI KWA KUNASWA NA SARE ZA JWTZ


JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limemkamata Saida Mohamed (30), mkazi wa Mwasonga Kigamboni, akiwa na sare za Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ). 


Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleimani Kova, alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa Agosti 31, mwaka huu, katika eneo la Mwasonga, Kigamboni.

Alisema Saida alikamatwa na suruali saba, mashati saba ya kombati, kofia 10, shati mbili nyepesi, fulana mbili na kofia moja aina ya bareti, vyote vikiwa mali ya JWTZ.

Alisema mtuhumiwa huyo, alikuwa na begi moja la kuwekea nguo za jeshi, cheo kimoja cha Koplo na mikanda miwili ya kijeshi.

Alisema uchunguzi unaendelea juu ya mwanamke huyo ili kubaini sababu za kumiliki sare za jeshi, kabla ya kufikishwa mahakamani.

Katika tukio jingine, polisi wamemkamata Husein Mkondoa (25), mkazi wa Gongolamboto Mzambarauni, akiwa anaendesha pikipiki huku akiwa amevaa nguo za kiraia na kofia ngumu ya kijani yenye nembo ya Polisi.

Alisema polisi walimtilia mashaka na kumkamata mtuhumiwa na anaendelea kuhojiwa.

“Naomba kutoa onyo kwa watu wote wenye silaha na sare za jeshi wazisalimishe kwa polisi au ofisi yoyote ya Serikali, msako wa kuwakamata wahalifu utakuwa endelevu na tutaingia nyumba hadi nyumba kuwatafuta wahalifu.

“Sambamba na operesheni hii, licha ya kubadilisha uongozi katika kituo cha Polisi Ubungo, tumeamua kutupia macho vitendo vya utapeli katika eneo la Ubungo Bus Terminal, ambalo watu wengi wanajifanya askari.

“Licha ya hilo, tumeunda kikosi cha kutumia video kamera na kamera za picha mnato ili kubaini na kuchukua hatua na nyendo mbalimbali ili kujenga ushahidi wa wahalifu hao wasiepuke mkono wa sheria,” alisema Kova.

Wakati huo huo, Jeshi la Polisi linawashikilia watuhumiwa wawili kwa kuchonga hati mbalimbali zinazotaka kufanana na za Serikali.

Kamishina Kova, aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Shadrack Samwel (27) mkazi wa Mbagala Sabasaba na Mwangi Samwel (38) mkazi wa Kimara Baruti.

Alisema watu hao, hawana ofisi maalumu hivyo hufanya shughuli hiyo sehemu yoyote na ofisi zao kuu ni mkoba pamoja na gari ambalo wanatembelea, lenye namba za usajili T 397 ADX aina ya Crester.

“Watuhumiwa hawa, tuliwakuta na mihuri 27 ambayo ni ya Serikali na taasisi binafsi, mihuri ya mawakili wa kujitegemea na wa serikalini, mhuri wa Jeshi pamoja na mhuri wa Serikali za mitaa.

“Pia tumewakamata na nakala mbalimbali za SUMATRA, ikiwemo karatasi za kukagulia magari, pleti namba za magari pamoja na nakala mbalimbali za ofisi hiyo,” alisema.

Katika hatua nyingine, polisi wanawashikilia watu watano, akiwamo Enea Dawsoni, ambaye ni mfanyakazi katika Kapuni ya Ndege ya Fast Jet, kwa jaribio la kutaka kupora fedha kiasi cha Sh 60,000,000 katika Kampuni hiyo.

Alisema watuhumiwa hao walinaswa katika Mtaa wa Samora na iligundulika walikuwa wana mawasiliano ya simu.

“Baada ya kuwakamata watu hawa, Polisi walielekea katika ofisi hizo na baada ya kufika walichukua simu ya watuhumiwa hao na kuona ujumbe mfupi wa maneno, ulioeleza kuwa fedha zipo karibu na chooni.

“Polisi walichukua simu ya wahalifu na walipopiga simu hiyo iliyokuwa na mawasiliano na majambazi hao, simu iliita kwa sauti kubwa ndani ya maungo ya mmoja kati ya watumishi wa Fast Jet.

“Mtumishi Enea Dawson alikuwa ameficha simu hiyo sehemu za siri katika nguo zake ambapo aliumbuka na kugundulika kuwa alikuwa na uhusiano wa karibu na majambazi hao,” alisema Kova.

 
Support : Copyright © 2011. HABARILINE - All Rights Reserved