JOPO la majaji watatu wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, limekataa pingamizi lililowekwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kutaka kampuni za simu zisiingie katika kesi ya kupinga tozo ya Sh 1,000 kwa mwezi kwa kila mmiliki wa laini moja ya simu.
Uamuzi huo ulitolewa jana na majaji hao; Lawrence Kaduri, Aloysius Mujuluzi na Salvatory Bongole, ambao sasa wameruhusu kampuni hizo za simu kujiunga katika kesi hiyo zikiwa walalamikaji namba mbili mpaka sita.
Katika pingamizi la kutaka kampuni hizo za simu zisiruhusiwe kujiunga katika kesi hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alikuwa akidai kuwa hana uhakika na mtu aliyeapa kwa niaba ya kampuni hizo kama alipewa mamlaka ya kufanya hivyo.
Upande wa Serikali uliweka pingamizi hilo dhidi ya kampuni ya Mic Tanzania yenye mtandao wa Tigo, Vodacom Tanzania, Airtel Tanzania, Zanzibar Telecommunication Limited (Zantel) na Tanzania Telecommunication Company Limited (TTCL).
Akisoma uamuzi huo, Jaji Bongole alisema hakuna hoja ya msingi ya kupinga kampuni hizo kuingia katika kesi hiyo. Mawakili wa kampuni za simu Fatma Karume na Beatus Malima, wameomba kufanya mabadiliko katika hati ya madai, ambapo wametakiwa wayawasilishe Jumanne ijayo na kesi ya msingi ya kupinga tozo hiyo ya laini za simu, itaendelea Oktoba 21, mwaka huu.
Kesi ya Msingi
Kesi ya msingi ilifunguliwa na Chama cha Kutetea Walaji, chini ya hati ya dharura kuomba Mahakama itangaze kuwa Sheria iliyopitishwa na Bunge inayotaka kila mmiliki wa laini moja ya simu ya mkononi kukatwa Sh 1,000 kila mwezi, ni kandamizi.
Taasisi hiyo inadai kuwa watumiaji wengi wa simu za mkononi, hawana uwezo wa kukatwa fedha hiyo kwa mwezi na kusisitiza kuwa sheria hiyo ikitekelezwa, itaathiri watumiaji wa huduma hiyo nchini.
Kwa mujibu wa madai ya chama hicho, sheria hiyo inakiuka matakwa ya Katiba ya nchi ya uhuru wa kupashana habari. Pia chama hicho kinataka Mahakama imzuie Waziri wa Fedha kupitia Mamlaka ya Mapato (TRA), kutoza kodi hiyo hadi maombi yao yatakapotolewa uamuzi.
TRA waendelea kudai
Mwezi uliopita TRA iliandikia waraka kwa kampuni za simu nchini kuzitaka zianze kukata kodi mpya ya laini mara moja.
Kodi hiyo mpya ilipitishwa wakati wa Bunge la Bajeti ya mwaka huu wa fedha wa 2013/2014, ambapo TRA katika waraka huo, imetaka utekelezaji wake uanze Julai 30, ili kusaidia shughuli za bajeti ya Serikali Kuu.
Kama kampuni hizo zikianza kutekeleza matakwa ya waraka huo, kila Mtanzania anayemiliki laini moja ya simu, atakuwa akidaiwa Sh 3,000 mpaka mwishoni mwa mwezi uliopita.
Mkurugenzi wa Elimu kwa Mteja, Huduma na Mapato wa TRA, Richard Kayombo, alikiri TRA kutoa agizo hilo lakini hakutaka kuzungumnia zaidi kwa kuwa tayari suala hilo liko mahakamani ambapo alisema si vema kuingilia uhuru wa mhimili huo wa Dola.
“Sitaki kuzungumzia kiundani sana suala hili, lakini ukweli ni kwamba kampuni hizi za simu zimeandikiwa waraka kuanza kulipa kodi na tumeandika kwa ajili ya utekelezaji wa kodi hii mpya,” alisema Kayombo.
source habarileo