Lusambo, ambaye ni mkazi wa kijiji cha Katumba -Azimo wilayani Sumbawanga alihukumiwa kutumikia kifungo hicho na Hakimu wa Mahakama hiyo, Adam Mwanjokolo, akiwa hayupo mahakamani hapo kwa kuwa alikuwa ameruka dhamana.
“Baada ya kusikiliza shauri hili upande mmoja na baada ya maombi maalumu kutoka kwa Mwanasheria wa Serikali kwa kuwa mshtakiwa ameruka dhamana, mahakama hii imeridhika na ushahidi wa upande wa mashitaka uliotolewa na mashahidi wanne akiwemo mtoto mwenyewe,” alibainisha Hakimu huyo wakati akisoma hukumu hiyo.
Hakimu Mwanjokolo aliamuru mtuhumiwa asakwe popote alipo na kuanza kutumikia kifungo mara tu atakapokamatwa. Awali Mwendesha Mashtaka, Mkaguzi wa Polisi, Thomas Kilakoi alidai mahakamani hapo kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Septemba 17 , mwaka jana, maeneo kati ya kijiji cha Katumba – Azimio na Ulinji wilayani Sumbawanga.
Siku moja kabla ya tukio hilo msichana huyo alienda kijiji cha jirani cha Ulinji kuhudhuria sherehe ya komunio hivyo alilazimika kulala kijijini hapo nyumbani kwa bibi yake ambapo siku iliyofuata alifuatana na mama yake mzazi na akina mama wengine kurejea makwao.
Kwa mujibu wa Mwendesha Mashtaka wakiwa njiani kurejea makwao ndipo mama mzazi wa msichana huyo alimwomba mshitakiwa aliyekuwa akiendesha baiskeli kuelekea kijijini Katumba -Azimio ampakie mtoto huyo kwenye baiskeli yake.
Inadaiwa kuwa mshitakiwa alikubali na kuondoka naye kuelekea kijijini Katumba -Azimio lakini kabla hawajafika kijijini hapo aliingia na kuanza kunywa pombe kwenye kilabu cha pombe huku akiwa amemwacha msichana huyo nje akiwa na baiskeli yake.
Mshitakiwa huyo anadaiwa baada ya kunywa pombe kilabuni humo aliamua kuendelea na safari akiwa amempakia msichana huyo kwenye baiskeli yake ambapo walipofika karibu na kichaka alisimama na kumuuliza msichana huyo kama anafahamu kuwa ameshakuwa mtu mzima.
Binti huyo alikana na kumweleza mshitakiwa kuwa yeye bado ni mtoto, ndipo alipomkamata kwa nguvu na kumpeleka kichakani na kuanza kumwingilia kwa nguvu huku akiwa amemziba mdomo kwa kitambaa alipomaliza kumtendea, unyama huo aliondoka na kumwacha mtoto huyo pale kichakani.