Kikao cha Bunge la Afrika Mashariki (EALA), jana kilivunjika kwa mara
ya pili baada ya Wabunge wa Tanzania, kutoka ndani ya ukumbi wakipinga
kanuni kuvunjwa juzi.
Baada ya wabunge wa Tanzania kutoka nje, Spika wa Bunge hilo,
Margareth Zziwa aliahirisha Bunge kwa dakika 15 ili kuweka mambo sawa,
lakini jitihada za kuwashawishi ziligonga mwamba na kuamua kuahirisha
Bunge hadi leo.
Hata hivyo, Mbunge wa Tanzania, Makongoro Nyerere hakuungana na wenzake
kugoma kwani alibakia ukumbini na kuungana na wabunge 32 wa Burundi,
Kenya, Uganda na Rwanda.
Awali, Mbunge Abdullah Ali Hassan Mwinyi alitoa msimamo wa wabunge wa
Tanzania kuwa walitoka, kupinga kitendo cha wabunge wengine kudharau
kiti cha Spika juzi na kutoka nje ili kushinikiza hoja yao.
Mwinyi alisema ili kushinikiza kuheshimiwa kiti cha Spika, wameamua
kutoka nje ya ukumbi huo kwa kuonyesha hawaungi mkono, tabia ya baadhi
ya wabunge kushinikiza hoja zao, kujadiliwa na Bunge hata kwa kukiuka
kanuni na taratibu.
“Jana(juzi) ilikuwa ni mara ya pili wenzetu, kudharau kiti cha Spika na
kutaka kutoa hoja na kujadiliwa bila kufuata kanuni, sasa tumeona ni
vizuri na sisi kwa kupinga kuvunjwa kanuni, tutoke ili kuonyesha
tunapinga mchezo huu,” alisema Mwinyi.
Mwinyi alisema kitendo cha wabunge wenzao kutoka nje ya ukumbi kwa
kukataliwa kuvunja taratibu, kinadhalilisha kiti cha Spika na hata
wabunge wenyewe.
Mbunge mwingine wa Tanzania, Twaha Taslima alisema kanuni zipo wazi kuwa
kama mbunge ana hoja na kutaka Bunge lijadili mambo ambayo si ya
dharura ni lazima aiwasilishe saa 24 kabla kwa Spika.
“Sasa jana(juzi), Mbunge wa Kenya, Peter Mathuki alitaka hoja yake ya
kutaka utaratibu wa kufanyika bunge kwa mzunguko ijadiliwe kitu ambacho
hakikuwa sahihi,” alisema Taslima.
Muthuki, juzi aliungwa mkono na nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), isipokuwa Tanzania.
Jana aliwasilisha hoja hiyo kwa kufuata utaratibu lakini haikujadiliwa baada ya wabunge wa Tanzania kutoka nje.
Katika hoja hiyo, msimamo wa wabunge wa Tanzania na Kamati ya Uongozi ya
Bunge ni kuwa vikao vyote vifanyike katika ukumbi wa Bunge, Arusha
baada ya kukamilika.
Wabunge wa Tanzania ambao jana walitoka ni Shyrose Bhanji, Profesa Nderakindo Kessy na Taslima. Wabunge wanne hawakuwapo.
Kwa mujibu wa kanuni za Bunge hilo, kama wabunge watatu wa nchi moja,
wakitoka nje kupinga jambo lolote basi kikao kinaahirishwa kwa dakika 15
na wasiporejea bunge linaahirishwa.
Akizungumzia mgogoro huo, Ofisa Habari wa EALA, Bobi Odiko alisema
kilichotokea jana si ukiukwaji wa taratibu na kuongeza kuwa ana imani
mambo yatakuwa sawa na vikao vitaendelea leo kwa amani.
-Mwananchi