Alisema kuwa kutokana na hali hiyo, atamshangaa
Rais Kikwete ikiwa atasikiliza kelele za wapinzani kwa sababu
walishirikishwa kupitia kamati na hata bungeni kabla ya kupitishwa
kwake.
“Nitamshangaa sana Rais Kikwete kama atashindwa
kusaini muswada huo kwa sababu ya kelele za wapinzani. Tuliwashirikisha
katika kila mchakato kabla na baada ya kuuwasilisha bungeni,” alisema
Chikawe.
Alisema kitendo cha wapinzani hao kujiunga pamoja
na kuanzisha kampeni za kuwahamasisha wananchi ili waukatae muswada
hakisaidii lolote, kwa sababu sheria zote zinatungwa bungeni na siyo
kwenye Viwanja vya Jangwani wala Ikulu.
Vyama vyampinga JK
Wakati Chikawe akisema hayo, viongozi wa Chadema,
CUF na NCCR-Mageuzi wameshikilia msimamo wao kwamba wataendelea kupinga
muswada huo uliopitishwa na Bunge, Septemba 6, mwaka huu.
Wakizungumza Dar es Salaam jana walipokutana na
Shura ya Maimamu ikiwa ni mwendelezo wao wa kukutana na asasi za kiraia,
viongozi wakuu wa vyama hivyo, walisema kamwe kasi yao ya kutaka
kutosainiwa kwa Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
haiwezi kupunguzwa kwa namna yoyote kwa kuwa wanatetea masilahi ya
Watanzania na siyo mtu binafsi.
Kauli yao imekuja siku moja baada ya Rais Kikwete
kusema kuwa baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakisema uongo kuhusu mchakato
wa Katiba unavyokwenda.
Wanasiasa pia hao wamepinga matumizi ya kauli za
kibabe kwenye mchakato huo na kuonya kuwa nguvu ya dola haiwezi
kushindana na nguvu ya umma.
Mbali na hayo, wanasiasa hao walisisitiza kwamba
hawatapiga magoti kuomba Katiba Mpya, kwani ni ya Watanzania wote na si
mali ya wanasiasa, chama cha siasa wala wabunge.
Rais Kikwete alikaririwa na magazeti mbalimbali
jana akipinga madai ya wapinzani kuwa hakuzingatia maoni yao wakati wa
uteuzi wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
“Nafahamu kwamba tunaambiwa tunasema uongo, lakini
ni vizuri ifahamike wazi kuwa hatuwezi kupunguzwa nguvu na kauli hizo
alizozitoa Rais Kikwete, kwani msimamo tulionao ni kuendelea kutetea
Watanzania,” alisema Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
Mbowe alimshauri Rais Kikwete atumie busara kwa kutosaini mkataba huo ili mchakato uende vizuri.
-mwananchi
-mwananchi