Johannesburg. Watanzania Agness Masogange na
Melisa Edward waliokamatwa kwa kutuhumiwa kubeba dawa za kulevya huko
Afrika Kusini wameachiwa kwa dhamana.
Mkuu wa Kitengo cha Dawa za Kulevya Afrika Kusini,
Kamishna Toto Mangaleni aliithibitishia Mwananchi jana kuwa watuhumiwa
hao wameachiwa kwa dhamana,lakini wataendelea kubaki Afrika Kusini
wakati kesi yao ikiendelea.
Mangaleni alisema wanawake hao ambao juzi pia
walipanda kizimbani, walipata dhamana hiyo jana kutoka Mahakama Kuu ya
Gauteng iliyoko eneo la Kempton Park jijini Johannesburg.
Hata hivyo, Kamishna Mangaleni alisema hawezi
kuzungumzia zaidi kuhusu kesi hiyo kwa sababu hataki kuharibu uchunguzi
ambao unaendelea dhidi ya Watanzania hao, ambao ni wasanii.
Marafiki wa karibu wa Masogange wanaoishi maeneo
ya Midland Johannesburg ambao walikataa kunukuliwa majina yao,
walithibitisha kuwa wanawake hao wameachiwa kwa dhamana.
“Ni kweli wameachiwa leo asubuhi. Lakini hatuwezi
kuongelea kwa kina habari hizi kwa sababu hatutaki matatizo na polisi.
Hii kesi bado inaendelea na wataendelea kubaki hapa hadi kesi yao
itakapomalizika,” alisema mmoja wa marafiki zake.
Naye Masogange aliandika kwenye mtandao wa ‘Facebook’.
“Namshukuru Mungu nimeamini wewe ulikuwa pamoja na
mimi katika maombi yangu na nashukuru kwa wote mliokuwa mkiniombea
Mungu kapokea maombi yenu.”
Masogange na Melissa walikamatwa Julai 2 mwaka huu
katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo jijini Johannesburg
wakiwa wana mabegi sita makubwa ya dawa zinazoaminika kuwa ni `Crystal
Methyl Amphetamine’.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Polisi cha Kuzuia na
Kudhibiti Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa aliiambia Mwananchi jijini Dar
es Salaam kuwa alikuwa amepata taarifa za kuachiwa kwa wasichana hao,
lakini alikuwa anawasiliana na watu wa Afrika Kusini ili kupata uhakika.
Nzowa, hata hivyo alilidokeza gazeti hili juzi
kuwa kuna uwezekano wanawake hao wangepata dhamana au kufungwa kifungo
chepesi kwani dawa walizokamatwa nazo ni kemikali zinazotumika
kutengeneza dawa za aina tofauti kwa matumizi ya binadamu ingawa pia na
dawa za kulevya.
Mamlaka yapinga uamuzi wa Mahakama
-mwananchi
-mwananchi