Home » » COASTAL UNION YAMSAINISHA MGANDA ALIYEZINYANYASA SIMBA NA YANGA KUTOKA URA

COASTAL UNION YAMSAINISHA MGANDA ALIYEZINYANYASA SIMBA NA YANGA KUTOKA URA


Klabu ya Coastal Union imekamilisha usajili wa mshambuliaji wa kiganda Yayo Lutimba kutoka timu ya mamlaka ya mapato ya Uganda URA. 

Aliyefanikisha zoezi hilo ni meneja wa Wagosi, Akida Machai ambaye amepanda ndege mpaka jijini Kampala kunasa saini ya kijana mdogo mwenye miaka 19, Yayo Lutimba Kato kutoka timu ya mamlaka ya mapato Uganda (URA).

Nassor Ahmed ‘Binslum’, ambaye ni mkurugenzi wa ufundi amesimamia kwa kiasi kikubwa kufanikisha usajili wa wachezaji takriban tisa ukijumlisha na Kato amezungumza na blog hii usiku wa leo baada ya Meneja Machai kuenda kumtambulisha Kato kwa Binslum na kuweka wazi kuwa tatizo la ukame wa mabao litaisha kwa wana Mangush.

Itakumbukwa kocha Mkuu wa Coastal Union, Hemed Morocco wiki chache zilizopita wakati wa kujiandaa na mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya URA, aliweka wazi bado kikosi chake kina matatizo ya umaliziaji.

Alibainisha kikosi hicho kipo vizuri kila idara kuanzia golikipa, mabeki na viungo ila hakuna mtu mwenye uchu wa mabao hivyo kuahidi kuwatumia wachezaji haohao kuwafundisha namna ya kuadhiri magolikipa wa timu pinzani.

Ndiyo maana winga Danny Lyanga alikuwa akichezeshwa namba kumi ili kumuangalia uwezo wake wa kupachika mabao lakini hakuonekana kucheza vema kwenye mechi ya URA.

Kwa usajili wa miaka miwili kuitumikia Coastal Union kinda huyu atakuwa na nafasi nzuri sana kujitengenezea jina nchini Tanzania hasa baaada ya kuwa na rekodi nzuri ya kuwafunga Simba na Yanga mabao mawili mawili katika mechi walizokutana nazo kwa vipindi tofauti.

Zipo taarifa kuwa Yanga nao walikuwa mbioni kumnyakua kinda huyu lakini Meneja Akida Machai amewazidi akili kwa kumfuata hukohuko kwao Uganda. Na hizi ni mbinu za ‘kimafia’ zinazotumiwa na timu kubwa duniani kote kunasa wachezaji mahiri.

Mungu akipenda kesho Kato ataungana na wachezaji wenzake katika kambi iliyopo pembezoni mwa bahari ya hindi Raskazone Hotel, jijini Tanga.

Wagosi wameanza vizuri mechi zao mbili za majaribio ambapo mechi ya kwanza walishinda bao 1-0 dhidi ya URA na siku tatu baadaye wakashuka dimbani dhidi ya Simba SC ambao nao walichapwa 1-0. Zipo taarifa za kucheza mechi ya kirafiki siku ya Eid pili uwanja wa Mkwakwani lakini zikishathibitishwa na timu tutakayocheza nayo tutawahabarisha.

TOA MAONI YAKO HAPA

 
Support : Copyright © 2011. HABARILINE - All Rights Reserved