Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), inatarajia kuvuna
kiasi cha Sh217.8 bilioni kwa mwaka, baada ya kuanzishwa kwa mfumo mpya wa
kulipa ada za magari kwa njia ya mtandao wa simu za mkononi na benki, unaoanza
leo.
Kabla ya kuanzishwa kwa mfumo huo, mamlaka
hiyo ilikuwa na uwezo wa kukusanya kiasi cha Sh147 bilioni kwa
mwaka.
Akizungmza na gazeti hili jana, Meneja
Mahesabu na Makusanyo ya Serikali katika mamlaka hiyo, Ramadhan Sengati alisema
ongezeko hilo ni sawa na asilimia 37 ya ongezeko la mapato
hayo.
Sengati alisema kiasi hicho ni mara mbili ya
makusanyo yaliyokuwa yakikusanywa kabla ya kuanzishwa kwa mfumo huo
mpya.
Alisema hatua hiyo inatokana na maboresho ya
mifumo ya kielektroniki ambayo TRA inaendelea kuyafanya ikiwa ni juhudi za kutoa
huduma bora kwa walipakodi.
“Hii ni pamoja na kuhakikisha kuwa mapato ya
Serikali yanakusanywa na yanawasilishwa kwa wakati kwenye mfumo mkuu wa Serikali
na benki kuu na kwamba kwa sasa TRA itakuwa inakusanya Sh217.8 bilioni sawa na
ongezeko la asilimia 37 kutoka Sh147 bilioni zilizokuwa zikikusanywa hapo awali
kabla ya kuwepo mfumo huu,” alisema.
Wiki iliyopita TRA ilitangaza kuanzisha
mfumo huo kwa lengo la kupunguza msongamano na wizi unaofanya na
vishoka.
Kuanzishwa kwa mfumo huo ni sehemu ya
jitihada za kutoa huduma bora kwa walipakodi na kuhakikisha kuwa mapato ya
Serikali yanawasilishwa kwa wakati.
Mkurugenzi wa Huduma na elimu kwa Mlipakodi
kutoka TRA, Richard Kayombo alisema mfumo huu utasaidia kumpatia taarifa ya
kiasi cha kodi anachotaka kulipa mteja.