Home » » SAKATA LA MADAWA YA KULEVYA,MASOGANGE NA MWENZAKE WAZIDI KUWAUMIZA VICHWA VIGOGO WA UNGA.

SAKATA LA MADAWA YA KULEVYA,MASOGANGE NA MWENZAKE WAZIDI KUWAUMIZA VICHWA VIGOGO WA UNGA.

BAADA ya hivi karibuni Taifa la Tanzania kutikiswa na tuhuma nzito ya biashara ya madawa ya kulevya, picha za watu wanaosafirisha bidhaa hiyo haramu kwa njia ya kumeza almaarufu kwa jina la punda, zimenaswa.
Picha hizo zinazopatikana mtandaoni ambazo hazikujulikana mara moja ni za watu kutoka nchi gani, zinaonesha jinsi madawa hayo yanavyoweza kusafirishwa kwa njia ya kuyameza tumboni huku madhara ya kufanya hivyo yakiainishwa.



MADHARA
Madhara makubwa yaliyoanishwa ni vijana wengi kupoteza maisha kwa urahisi wakati wakihitaji utajiri wa haraka.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyoambatanishwa na picha hizo, watu wanaobeba madawa ya kulevya kwa njia hii wako katika hatari kubwa ya kuweza kuharibu utumbo na kusababisha vifo vya ghafla.
Hali hiyo huweza kutokea pindi madawa hayo yatakapokaa kwa muda mrefu tumboni na kupasuka kutokana na kuchelewa kutolewa.


Mfano watolewa
Katika maelezo ya picha hizo, inadaiwa mmoja wa watu waliokuwa wakifanya kazi hiyo ya ‘upunda’ alipasukiwa na madawa hayo tumboni na kujikuta akifariki dunia baada ya kuchelewa kuyatoa.
Mwingine ilidaiwa kuwa, aliumbuliwa na mashine zilizokuwa kwenye uwanja wa ndege (haukutajwa ni wa nchi gani) na ililazimika  kufanyiwa upasuaji kisha madawa hayo kutolewa.


SAFARI ZA NDEGE HUCHANGIA

Kitu kikubwa ambacho kimekuwa kikiwasababishia vifo wabebaji wengi ni kuahirishwa au kucheleweshwa kwa safari zao za ndege zinazosafiri katika mataifa mbalimbali duniani.

Hali hii huweza kutokea wakati wowote kutokana na hali ya hewa kuchafuka au dharura nyinginezo na kuwakuta wabebaji hao wakiwa hawana ujanja wa kuweza kukwepa  vifo.

WAFANYABISHARA, WANASIASA WATAJWA

Katika hili watu wanaotajwa kuwabebesha madawa ya kulevya vijana wa Kitanzania na kuwatuma kuyapeleka katika nchi mbalimbali duniani ni wafanyabishara wakubwa na wanasiasa.

Tuhuma hizi zimekuwepo kwa muda mrefu kwamba vigogo hao huwatumia vijana wa Kitanzania kuhatarisha maisha yao ilhali wao wakitajirika kwa kupata fedha nyingi.

Majina makubwa ya viongozi na watoto wa vigogo yamekuwa yakitajwa kuhusika kwa namna moja ama nyingine na biashara hiyo haramu na wengi hawajitokezi hadharani kukanusha.

PUNDA WAKUBWA NI WASANII

Punda wakubwa ambao wanatumika kwa ajili ya kubeba madawa ya kulevya ni wasanii wa filamu na wale wa muziki ambao mara kwa mara huonekana wakisafiri nchi mbalimbali duniani.

Inadaiwa wasanii hutumika kwa urahisi kufanya biashara hiyo kwa kuwa ni  vigumu kutiliwa shaka pindi wanapokuwa wanapita kwenye viwanja vya ndege huku wakiwa wamemeza madawa hayo.

Aidha, wasanii wanatumika kwenye biashara hiyo kwa kuwa ni watu wa kusafirisafiri sana kwa shughuli zao za kisanii na pia jamii duniani kote inawapenda, hivyo wana uwanja mpana wa kusaidiwa pindi wanapopata matatizo.

Mtego mwingine wa wasanii unaowafanya kuingia katika  biashara hiyo ni wengi wao kutaka kuishi kifahari tofauti na uwezo wao, hivyo hukubali kuwa punda ili kuweza kupata kipato zaidi  ya kile wanachokipata katika  kazi zao.

Masogange na mwenzake wawaumiza vigogo

Huku hali ikiwa ni ya sintofahamu, baadhi ya vigogo wanaodaiwa kuhusika na biashara hiyo hapa Bongo wanaumia vichwa hasa baada ya msanii, Agnes Gerald ‘Masogange’ (pichani) na mwenzake Melisa Edward kukamatwa nchini Afrika Kusini wakihisi wakati wowote wanaweza kuwataja.

Masogange na mwenzake huyo wanaendelea kuhudhuria mahakamani nchini huko na wakizidiwa wanaweza kuwataja watu waliowatuma kwa kuwa ni vigumu kwao kupitisha  madawa hayo Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere jijini Dar bila ya msaada wa vigogo wenye uzoefu wa biashara hiyo.

Iwe fundisho

Picha zinazowaonesha watu waliokufa kwa kumeza ili kusafirisha madawa ya kulevya na kupoteza maisha yao huku wengine wakiathirika kwa kiasi kikubwa, ziwe fundisho kwa vijana wa Kitanzania ambao wamekuwa wakifanya madili hayo na wale wanaotamani kufanya wajue kwamba kujiingiza huko ni kujitafutia vifo.

TOA MAONI YAKO HAPA

 
Support : Copyright © 2011. HABARILINE - All Rights Reserved