Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kitaifa, Bernard Membe, ameongoza mamia ya waombolezaji
katika kuaga mwili wa Meja Khatib Mshindo aliyefariki dunia
Agosti 28, mwaka huu baada ya kuangukiwa na bomu huko Jamhuri ya
Demokrasia ya Congo (DRC). Bomu lililomuua ofisa huyo wa JWTZ aliyekuwa
katika misheni ya Umoja wa Mataifa ya Kulinda Amani, lilipuliwa na waasi
wa M23.
Kifo cha ofisa huyo kimekuja siku 47 tangu kuuawa kwa bomu, wapiganaji wengine saba wa Tanzania huko Darfur.
Wapiganaji hao walishambuliwa na kundi linaloaminiwa kuwa la Janjaweed.
Maombolezo ya jana yalifanyika katika Viwanja vya
JWTZ Lugalo jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali
wa JWTZ.
Akitoa Salam za rambi rambi, Waziri Membe alisema taifa limempoteza shujaa aliyekuwa akitekeleza majukumu yake nchini DRC.
“Tumempoteza mtu shujaa, alikuwa akitekeleza
majukumu yake nchini DRC, Serikali haitaweza kumsahau, kwa sababu
alikuwa miongoni mwa mashujaa waliokufa kazini,” alisema Membe.
Alisema kifo hicho kimeifanya taifa kumwaga damu
ya kishujaa na kwamba waliobaki hawarudi nyuma na badala yake, watakuwa
na ari ya kusonga mbele katika mapambano. “Waliobaki wataendelea
kushika mpini kwa ajili ya kuwatetea wananchi wa nchi hiyo ambao
wamekata tamaa ya maisha kutokana na vita vinavyoendelea katika nchi
yao,” alisema.
Waziri huyo alisema watu wanaoathirika katika nchi zenye vita ni wanawake na watoto.
Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis Mwamunyange alisema, marehemu alifariki dunia akiwa njiani wakati akiwahishwa hospitalini.
Alisema waasi wa M23 walirusha bomu
lililosababisha kifo cha marehemu na kujeruhi watu wengine watano ambao
mpaka sasa wanaendelea na matibabu.
Jenerali Mwamunyange alisema JWTZ litaendelea
kuwakumbuka marehemu hao na kuwaombea majeruhi ili waweze kupona haraka
na kurejea kwenye majukumu yao Alisema kuwa, marehemu alikuwa akifanya
kazi katika kikosi cha mizinga 83 KJ kilichopo Kibaha Pwani. Mwili wa
marehemu ambaye ameacha mjane na watoto watatu, umesafirishwa kwenda
Zanzibar kwa ajili ya maziko.