KWELI
dunia inakwenda ukingoni, mwanamke mmoja anayedaiwa kuwa ni mke wa mtu,
amefanya kitendo cha kinyama baada ya kujifungua msalani na kukiua kichanga chake.
Tukio hilo limetokea hivi karibuni maeneo ya Mazizini, Ukonga Wilaya ya
Ilala jijini Dar es Salaam baada ya mwanamke huyo ambaye jina lake
halikupatikana kukitumbukiza kichanga hicho chooni.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, mwanamke huyo ni mkazi wa Ukonga Moshi Bar
alidaiwa kunywa dawa kwa ajili ya kuutoa ujauzito aliokuwa nao wa miezi
minane na baada ya kuona hali imebadilika alitoka nyumbani kwake Moshi
Bar na kukimbilia Ukonga Mazizini kwa ajili ya kutaka msaada kwa mama
yake mdogo.
Baada ya kufika kwa mama yake mdogo aliomba maji kwa ajili ya kwenda
chooni, hata hivyo alizunguka nyuma ya choo kwa ajili ya kujipa msaada
wa siri lakini hali ilivyokuwa mbaya zaidi, aliamua kuingia ndani ya
choo hicho na kujifungua kichanga hicho na kukidumbukiza ndani ya shimo
la choo.
Mashuhuda
wa
tukio hilo walisema kuwa walimuona mwanamke huyo akibebwa kwenda ndani
kwa mama yake mdogo ili aweze kupatiwa msaada zaidi lakini hali ilizidi
kuwa mbaya kwa kuanza kuvimba mwili kutokana na kutokwa na damu
nyingi.
Waandishi wetu walifanikiwa kuzungumza na mama mdogo wa mwanamke huyo
ambaye alijitambulisha kwa jina la mama Athony alikiri binti huyo
kukumbwa na mkasa huo wakati yeye akiwa kwenye shughuli zake.
“Kweli nafahamu, alikuwa ni mjamzito na alifika nyumbani kwangu saa tano
asubuhi, alichokifanya hapa si kitu cha bahati mbaya ni makusudi,” alisema mama huyo.
Mama Antony alisema kuwa wakati anarudi nyumbani aliukuta umati wa
watu na alipoingia ndani ndipo alipopewa habari za tukio hilo.
Alipotakiwa kutaja jina la binti huyo, mama huyo alianza kuangua kilio
na kuwafanya waandishi wetu washindwe kuendelea na mahojiano naye.
Mwakilishi wa mjumbe na shina namba 34 Ukonga Mazizini, Bi Mtende
alisema kuwa tukio hilo limewashangaza kutokana na mwanamke huyo kwenda
kutupa kichanga chooni kwa makusudi.
Bi Mtende alisema kwanza mwanamke huyo siyo mkazi wa maeneo hayo, hivyo hakuna aliyeweza kumjua kwa jina.
Kikosi cha zimamoto na uokoaji kilifika katika eneo hilo majira ya saa saba mchana kwa ajili ya kutimiza wajibu wao
Kikosi hicho kikiwa kimesheheni zana za uokoaji kilikuta kichanga hicho
kikielea chooni na kwa kutumia mbinu zao za uokoaji na walifanikiwa kukitoa kichanga hicho kikiwa maiti.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, ACP Marietha Minangi
alikiri kutokea kwa tukio hilo ambalo yeye aliliita ni la kikatili na
mwanamke huyo amepelekwa katika Hospitali ya Amana kwa matibabu na mwili
wa kichanga hicho kimepelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa
uchunguzi zaidi.
Waandishi wetu walifika katika Hospitali ya Amana kwa ajili ya kupata mahojiano na mama huyo Jumanne iliyopita.