SIKU chache baada ya kukamatwa kwa
askari 'feki' wa Usalama Barabarani mwenye cheo cha Sajini, akifanya kazi ya
kuongoza magari eneo ya Tabata Kinyerezi, Dar
es Salaam, mambo mapya yamezidi kubainika juu ya
sababu za mtu huyo kujiingiza katika kazi hiyo bila kutambuliwa na Jeshi la
Polisi.
Habari
zilizolifikia gazeti hili kutoka vyanzo vya kuaminika, zinasema trafiki huyo
'feki', ambaye inadaiwa jina lake
halisi ni James Juma
Hussein (45), mkazi wa Kimara Matangini, alianzia kazi hiyo mkoani Singida
kabla ya kujipa uhamisho wa kikazi kwenda Dar es Salaam.
Chanzo
chetu kilieleza kuwa, trafiki huyo alikuwa na shemeji yake aliyeitwa Shaban
ambaye aliajiriwa na Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani aliyekuwa
akifanyia kazi mkoani Tabora.Vyanzo
vyetu viliongeza kuwa, baada ya shemeji yake kufariki mkoani Tabora, trafiki
huyo alipata mwanya wa kuchukua nguo za kazini alizokuwa akizitumia shemeji
yake.
Inadaiwa
trafiki huyo 'feki', aliwahi kupata mafunzo ya upolisi katika Chuo cha Polisi
Moshi (CCP), mkoani Kilimanjaro lakini alifukuzwa.Chanzo
hicho kiliongeza kuwa, baada ya ndugu wa trafiki huyo kufariki dunia, trafiki
'feki', alikuwa akifanya kazi hiyo bila ndugu zake kujua akianzia mkoani
Singida bila kushtukiwa.
"Jamaa aliamua
kujirithisha kazi ya shemeji yake, alikwenda Singida na kufanya kazi hiyo kwa
muda usiojulikana," kilisema chanzo chetu.Chanzo hicho
kiliongeza kuwa, kutokana na uchache wa matrafiki mkoani Singida, aliingiwa
hofu ya kuweza kujulikana; hivyo aliamua kujipa uhamisho wa kwenda jijini Dar es Salaam.
"Akiwa Dar es Salaam, alifanya
kazi hii kwa muda mrefu bila kujulikana hadi alipokamatwa wiki iliyopita akiwa
eneo lake la kazi akiongoza magari," kilisema chanzo hicho.Mtoa habari huyo
alisema polisi walianza kumtilia shaka trafiki huyo kutokana na adhabu zake
alizokuwa akizitoa kwa madereva.
"Tulianza kuwa
na hofu naye kwa sababu yeye adhabu zake kwa kila dereva aliyekuwa akimkamata
alimtoza sh. 20,000 hadi 25,000," kilieleza chanzo hicho.Sababu nyingine
iliyowafanya polisi wamtilie shaka ni utamaduni wake wa kuondoka mapema kwenye
kituo cha kazi ambavyo alikuwa akijipangia mwenyewe.
"Trafiki akiwa
kazini, inabidi awe kituoni kwake kuanzia asubuhi hadi jioni muda wa kazi
unapomalizika, tulishangaa kuona mwenzetu anaingia kazini asubuhi na kuondoka
kabla ya muda wa kazi," kiliongeza chanzo hicho.Inadaiwa trafiki huyo
alikuwa akifanya hivyo baada ya kukamilisha mahesabu yake aliyokuwa amejiwekea
ambapo hali hiyo iliwafanya polisi waanze kujiuliza maswali na ndipo walipoanza
kumfuatilia.
Baada ya kufuatiliwa
bila yeye kujua, walibaini hata upigaji wake wa saluti ni utata mtupu ambapo
kutokana na hali hiyo, waliweka mtego na kufanikiwa kumkamata.
Hadi sasa anaendelea kushikiliwa na Jeshi la
Polisi ambalo limeahidi kutoa taarifa kamili baada ya uchunguzi wao kukamilika.