Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe akizungumza na
waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu hali ya vurugu
zinazoendelea Mtwara katika sakata la mradi Gesi asilia kuja Dar es
Salaam.PICHA NA VENANCE NESTORY
Dodoma: Wabunge
Wawili Maarufu wa Chadema, Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini) na Godbless
Lema (Arusha Mjini) wameingia katika vita ya maneno ambayo chanzo chake
ni kauli ya Lema aliyotoa katika kikao cha wabunge (briefing)
kilichofanyika mjini Dodoma Jumanne wiki hii.
Lema akizungumza katika kikao hicho, anadaiwa kutoa maneno ambayo
yalitafsiriwa na wabunge wengi kuwa yalikuwa yakimlenga Zitto kuhusu
hatua yake ya kukataa posho na kumtuhumu kwamba ana ukwasi ambao
unapaswa kuhojiwa.
Gazeti hili lilimtafuta Lema likirejea taarifa iliyotolewa na Zitto
akilalamika kwamba Lema alimshambulia katika kikao hicho cha wabunge
wote na kwamba alikuwa akimlenga yeye.
Lema, hata hivyo, alikiri kuzungumzia suala hilo akisema:
“Mimi sikumtaja mtu, kwahiyo kama kuna mtu analalamika hilo ni suala jingine, ila mimi nilimaanisha nilichokisema”.
Hata hivyo, Zitto alieleza kuwa msimamo wa Lema ulikuwa unapingana na
wabunge wengine wa Chadema, ambao waliwahi kupendekeza kuwa posho
zifutwe.
Zitto alisema kuwa yeye mwenyewe, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu
Lissu na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika waliwahi kupendekeza kuwa posho
zifutwe.
“Mimi sipokei posho kabisa, posho za vikao na ndiye mbunge pekee ambaye
hapokei posho ya vikao tangu mwaka 2011,” aliongeza Zitto, ambaye
anahudhuria mkutano unaozungumzia uendeshaji wa Serikali kwa uwazi huko
London, Uingereza.
Zitto alisema malipo ya wabunge mpaka sasa ni makubwa sana ukilinganisha
na hali ya wananchi wakati Serikali ikishindwa kulipa vizuri walimu na
wauguzi.
“Hatuwezi sisi kama wabunge kuanza kulilia posho, wakati wananchi wetu
hawana maji, hatuwezi kulilia posho. Mbunge anayetaka posho zaidi
akafanye kazi nyingine na awaachie wanaoweza kuwakilisha watu
waendelee,” alisema Zitto.
Lema, hata hivyo, alisema kwamba katika mkutano huo aliweka bayana
kwamba umasikini siyo uzalendo na kusisitiza kuwa wabunge wanapaswa kuwa
na maslahi bora na wakati huohuo wana wajibu wa kuwatetea watumishi
wengine wa umma.
“Nilisema huwezi kuzuia taasisi moja kupewa maslahi bora eti tu kwa
sababu watumishi wengine hawalipwi vizuri, ni haki wabunge kulipwa
vizuri na wakati huo wapiganie maslahi ya watumishi wengine,” alisema
Lema na kuongeza:
“Kwahiyo nikasisitiza kwamba nawashangaa wale ambao wanakataa posho ya
Sh80,000 na ukienda kuchunguza wanakatwa fedha zote kutokana na mikopo
waliyochukua, lakini bado wakija sehemu kama Arusha wanalala kwenye
hoteli ya gharama kubwa kati ya Dola za Marekani 150 na 600”.
Alisema katika mazingira hayo kunakuwapo maswali mengi yasiyokuwa na
majibu na kwamba mbunge wa aina hiyo alitakiwa anapokuwa katika mji
wowote nchini aishi katika hoteli yenye thamani kati ya Sh20,000, 30,000
na hata Sh50,000.
“Kwa hiyo ikiwa unakataa posho ya Sh80,000 halafu unalala chumba cha
Dola 600 hustahili kupata credibility (sifa) stahili, ni unafiki tu na
kutafuta sifa za kipuuzi,”alisema Lema.
Alisisitiza kwamba wabunge wa Tanzania hawalipwi ipasavyo na kwamba
kudai malipo ya ziada hakuwaondolei wajibu wao wa kuwatetea watumishi
wengine wa umma ambao pia malipo yao ni kidogo.
“Kuna hatari ya kuona kwamba Sh80,000 au Sh200,000 ni fedha nyingi, ni
kwamba kama sisi wabunge tutalipwa Sh50,000 basi maana yake ni kwamba
walimu au polisi tutaridhika wakilipwa hata Sh10,000,”alisema
Mwananchi