Home » , , » WABUNGE WATAKA KULIPWA KIINUA MGONGO BAADA YA KAMPENI ZA KUWANIA WADHIFA HUO! ,KISA CHA KAULI HIYO HIKI HAPA

WABUNGE WATAKA KULIPWA KIINUA MGONGO BAADA YA KAMPENI ZA KUWANIA WADHIFA HUO! ,KISA CHA KAULI HIYO HIKI HAPA

KAULI ya Spika Anne Makinda, kwamba hali za wabunge huwa mbaya baada ya ubunge kukoma, imeonesha kuwauma baadhi yao ambao wamekiri kwamba ina ukweli. Baadhi ya wabunge hao wamefikia hatua ya kupendekeza wasilipwe kiinua mgongo, mpaka wamalize kampeni za kuwania kiti hicho baada ya muda wao kuisha, ili wasipochaguliwa, kiwasaidie kusogeza maisha mbele.
Wakizungumza na gazeti hili Ofisi Ndogo ya Bunge jana, baadhi yao walisema siasa ni jambo la ajabu, kwani aingiapo mtu hawezi kusema unaacha kugombea, ni sawa na kuathirika na jambo fulani kama vile mtumia dawa za kulevya.
“Ukiingia kwenye siasa, huwezi kusema unatoka, unakuwa mlevi sawa na mtumia dawa za kulevya, huwezi kuacha ndio maana hata sisi wabunge hatuwezi kuacha kugombea,” alisema Mbunge wa Bukene, Selemani Zedi (CCM) alipozungumza na gazeti hili katika ofisi ndogo za Bunge jana.
Mbunge wa Namtumbo, Vita Kawawa (CCM), alisema awamu ya ubunge inapokoma, hupewa Sh milioni 60 kama kiinua mgongo na kudai kuwa fedha hizo sio nyingi kwa kuwa hutumiwa kuendesha kampeni katika uchaguzi.
“Kiinua mgongo sio kikubwa, kinatofautiana na awamu, mfano mwaka 2010 ilikuwa Sh milioni 60, sasa unapewa wakati ndio unakwenda kwenye kampeni, unakuta unazitumia zote, halafu unakosa ubunge, hapo ndio dhiki zinaanza,” alisema Kawawa.
Alimshukuru Spika Makinda kwa kulisema hilo kwani maisha baada ya ubunge huwa magumu kwa kuwa hawana pensheni na kama Mbunge hana biashara au shughuli za kilimo, maisha ndio hapo yanaanza kudorora. Mbunge wa Ole, Rajabu Mbarouk Muhammed (CUF), alisema hali ya wabunge wengi mara baada ya ubunge kukoma ni mbaya, kwa kuwa fedha wanazopata wakiwa wabunge, huzitumia na wananchi katika majimbo yao.
“Tunaomba utaratibu wa kupewa pensheni uwepo, hali sio nzuri kwa wabunge mara baada ya ubunge kukoma, kwa kuwa fedha tunazopata tunazitmia na wananchi kwenye kazi za maendeleo ya jimbo,” alisema Mbarouk.
Kawawa naye alisema tofauti na ilivyo katika mtazamo wa wananchi kwamba wabunge wana fedha nyingi, lakini hawana fedha na kidogo wakipatacho mara nyingi hukitumia kwenye majimbo yao, wakiamini uchaguzi mwingine ukija watachaguliwa.
Akizungumzia Mfuko wa Jimbo, Kawawa alisema fedha za Mfumo wa Jimbo sio nyingi kama wananchi wanavyodhani na kwamba zinatumika kwenye miradi katika majimbo husika, na wakati mwingine wanaingia mifukoni mwao kutoa fedha za miradi ya wananchi au kusaidia wananchi.
“Inafika mahali tunasahau hata familia, wake au waume zetu… tunapeleka fedha majimboni kusaidia wananchi. Wengine wanakulilia mpaka ada za watoto na mambo mengine,” alisema Kawawa.
“Mfano jimboni kwangu mfuko wa jimbo nimepata Sh milioni 47, nina kata 16, hivyo kila kata ninaipa Sh milioni tatu, hebu niambie zitajenga mradi gani kama sio mbunge kuingia mfukoni na kusaidia?” Alihoji Zedi.
Mbarouk (CUF), alikwenda mbali na kusema Spika amefikia kutamani wabunge wawe wajasiriamali, kutokana na utendaji mbovu wa baadhi ya watendaji wa halmashauri wanaofuja fedha za umma na kushindwa kufikia malengo.
“Haiwezekani sisi tuonekane tumechoka hoi mpaka Spika wetu anafikiria kutusaidia tuwe wajasiriamali kwa sababu ya uzembe wenu. (Watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe wanaodaiwa kupoteza Sh milioni 273 zilizolekezwa kwa matumizi ya shughuli za maendeleo katika halmashauri hiyo.)
“Tunaonekana tumechoka kwa kuwaza majibu kwa wananchi ya mambo ambayo fedha imetengwa baada ya kuyapigia kelele na kupitisha bajeti bungeni, kwa kweli tutabanana mpaka kieleweke,” alisema Mbarouk.

TOA MAONI YAKO HAPA

 
Support : Copyright © 2011. HABARILINE - All Rights Reserved