WATU sita wamelazwa katika Hospitali ya DDH-Bunda, mkoani Mara, kutokana na kujeruhiwa vibaya kwa kile kinachodaiwa ni kupigwa na askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ambao wanaendesha operesheni ya kusaka wawindaji haramu.
Mganga Mkuu katika wodi ya wanaume hospitalini hapo, Dk. Alphonce Kwessi, alisema kuwa majeruhi waliopokewa hospitalini hapo ni pamoja na Diwani wa Kata ya Nyarikoba wilayani Tarime, Mustapha Mashani, wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambaye ameruhusiwa baada ya hali yake kutengamaa.
Dk. Kwessi alisema kuwa majeruhi wengine ambao bado wamelazwa ni pamoja na Mwenyekiti wa Kijiji cha Kipaso wilayani Tarime, Robert Mrenda (CCM), Saguda Mihayo, Makoye Kazi, Ezekiel Nyarusi na Igeye Wambura.
Alisema kuwa majeruhi hao wamefikishwa hospitalini hapo tangu Oktoba 16, mwaka huu wakiwa na hali mbaya na kwamba waliletwa na askari hao pamoja askari wa Tanapa, wakidai kuwa wamekamatwa kwa tuhuma ya uwindaji haramu.
Hata hivyo diwani huyo wa CHADEMA juzi alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Bunda na kushitakiwa kwa uwindaji haramu, ambapo alipatiwa dhamana baada ya kutimiza masharti.
Kutokana na suala hilo, Mratibu wa Mafunzo Kanda ya Ziwa Mashariki wa CHADEMA, Chacha Heche, juzi alifika hospitalini hapo, alisema chama chao hakiridhiki kabisa na nguvu kubwa iliyotumika katika kuwakamata watu hao.
Heche alisema kuwa wapo watu waliokamatwa bila kuwa na vielelezo wakati wakiwa majumbani mwao, akiwamo diwani huyo.
“Haturidhishwi na nguvu kubwa iliyotumika na mamlaka inayofanya kazi ya kusaka wawindaji haramu kiasi cha kukiuka na kuvunja miiko na taratibu za haki za binadamu,” alisema.
Alisema kuwa wao kimsingi hawapingi zoezi hilo la kukamata wawindaji haramu lakini inabidi liangaliwe upya, kwani nguvu inayotumika katika kukamata watuhumiwa ni kubwa mno, ikiwa ni pamoja na watuhumiwa kupewa adhabu za kijeshi.
“Huu ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, watu wamekamatwa bila kuwa na vielelezo, tena wengine majumbani mwao, kwa mfano diwani huyu, lakini baada ya kukamatwa walifichwa kwenye kambi mbalimbali, wamepigwa sana, yaani ukiwaona utashangaa, wamesema eti walikuwa wanapewa adhabu za kijeshi,” alisema.
Polisi wilayani Bunda walithibitisha kuwapo kwa majeruhi hao, hawakuwa tayari kutoa taarifa zaidi kwa madai kuwa ni operesheni ya kitaifa.
SOURCE .TANZANIA DAIMA