Ni
kawaida kwa watoto kulia. Hata watoto wanaozaliwa na afya njema kabisa
wanaweza kulia kwa jumla ya wastani wa kati ya saa moja mpaka matatu kwa
siku. Kwa vile watoto hawawezi kujifanyia chochote wao wenyewe zaidi ya
kutegemea wazazi, walezi ama watu wengine wanaowazunguka katika
kuwapatia chakula, joto, na faraja, kilio ni njia ya mtoto ya
kuwasilisha moja ya mahitaji hayo.
Hata hivyo, kwa kadiri siku
zinavyopita mzazi mpya ataweza kutambua kuwa kilio cha mtoto wake
kinamaanisha anahitaji nini kutokana na mfumo wake wa kulia.
Kadiri
watoto wanavyokua ndivyo ambavyo hujifunza hatua mbalimbali za
kuwasiliana na wazazi ama walezi wao. Wanakuwa na namna nzuri ya
kuwasiliana kwa mfano kwa macho, na kutoa sauti, na hata kutabasamu
ambavyo vyote kwa pamoja hupunguza haja ya kulia.
Sababu zinazofanya watoto kulia
Tuangalie sababu kadhaa zinazosababisha mtoto kulia na nini anachotakiwa mzazi ama mlezi kufanya pindi mtoto anapolia.
1. Hitaji la chakula
Njaa
ni mmoja ya sababu kubwa inayowafanya watoto wengi kulia. Uwezekano wa
mtoto kulia unaendana sana na umri wa mtoto. Kadiri jinsi mtoto alivyo
mdogo zaidi ndivyo uwezekano wa kulia sana pindi anapohisi njaa
unavyokuwa mkubwa, isipokuwa katika siku mbili za mwanzo baada ya
kuzaliwa ambapo watoto hula kwa kiasi kidogo sana.
Kwa kawaida katika
siku mbili za mwanzo tangu mtoto kuzaliwa, maziwa ya kujilimbikizia
mapema sana yaani ‘colostrum’ huwa ni kidogo sana kwa mama walio wengi
na huanza kuongezeka kuanzia siku ya tatu baada ya kujifungua.
Pia tumbo
la mtoto katika kipindi hiki huwa bado dogo sana na hivyo uwezo wake wa
kuhifadhi maziwa anayonyonya huwa bado mdogo hali ambayo humfanya mtoto
kujisikia njaa. Hivyo kama mtoto wako analia, uwezekano mkubwa ni kuwa
ana njaa na hivyo mzazi unashauriwa kumnyonyesha.
Inawezekana mtoto
asiache kulia mara moja, lakini mama unashauriwa kuendelea kumnyonyesha
taratibu na mtoto anaweza kuacha kulia kwa kadiri anavyoburudika na
chakula na kuanza kushiba. Iwapo mama unadhani mtoto wako ameshiba
lakini bado anaendelea kulia, inawezekana kuna sababu nyingine zaidi.
2. Hitaji la starehe
Baadhi
ya watoto wanakuwa na hisia kali pindi vitu kama nguo inapoelekea
kumbana sana au iwapo anahisi kuna kitu chochote ndani ya nguo yake
kinachomsababishia maumivu. Wapo baadhi ya watoto ambao hawaoneshi
kuhangaika pale nepi zinapokuwa zimelowa sababu ya mkojo au kinyesi, kwa
vile baadhi yao huihisi joto na hivyo kupendezewa na hali hiyo, wakati
watoto wengine hulia na kuhitaji kubadilishwa nguo walizovaa mara moja,
hasa kama ngozi zao laini zinasumbuliwa.
Ni vyema kwa mzazi ama mlezi
kumchunguza mtoto wako kama amechafua nepi na kumbadilisha. Vilevile ni
vyema kuangalia kama nguo alizovikwa hazibani na hakuna chochote ndani
ya nguo kinachomletea maumivu.
3. Hitaji la kuwa na joto la wastani
Baadhi
ya watoto hawapendi kubadilishwa nepi au kuogeshwa. Hawajazoea kuhisi
hewa yenye joto tofauti juu ya ngozi zao. Wengi wao hupendelea sana kuwa
na hali ya jotojoto lililohifadhiwa. Kwa hiyo ni vyema kumbadilisha
mtoto nepi haraka ili kuweza hifadhi joto lake. Inashauriwa pia
kutokumvalisha nguo nyingi zaidi ya mahitaji ili mtoto asije akahisi
joto zaidi ya analolihitaji mwilini na hivyo kupelekea kuanza kulia.
Inashauriwa
pia kutomfunika mtoto kwa mashuka au mablanketi mengi hasa wakati wa
kumlaza. Kabla ya kuamua ni kiasi gani cha nguo unachohitaji kumfunika
mtoto wakati wa kulala, ni vyema kuangalia kama mwili wa mtoto ni wa
moto au baridi isivyo kawaida. Unaweza kufanya hivi kwa kuhisi joto la
tumbo lake kwa kutumia kiganja chako.
Iwapo mtoto ana joto sana,
unashauriwa kupunguza idadi ya nguo za kumfunika vivyo hivyo iwapo
unahisi mtoto ana baridi isivyo kawaida inashauriwa kuongeza idadi ya
nguo za kumfunikia. Usipime joto la mwili wa mtoto kwa kutumia joto la
mikono au miguu yake kwani si kitu cha uhakika na mara nyingi huleta
matokeo yasiyo sahihi kwa vile ni kawaida ya mikono au miguu ya watoto
kuwa ya baridi.
4. Hitaji la kushikwa ama kubebwa
Baadhi
ya watoto wanahitaji kuwa karibu na wazazi wao kwa kubebwa na
kubembelezwa. Watoto wakubwa wanapata faraja kwa kuwaona wazazi wao
wakiwa karibu na kusikia sauti zao, lakini mara nyingi watoto wachanga
wanahitaji kushikiliwa na kubembelezwa kwa faraja. Kama umemlisha mtoto
wako na kumbadilisha nepi wakati mwingine mtoto anahitaji kubebwa pia.
Baadhi
ya wazazi uhofia kuwa wanaweza kuwaharibu watoto wao kimakuzi pindi
wanapowabeba sana. Hiyo si kweli hususani kwa miezi michache ya mwanzo
tangu kuzaliwa kwa mtoto. Wakati baadhi ya watoto hawapendi kubebwa,
wapo wengine ambao hutaka kubebwa karibu muda mwingi. Iwapo mtoto wako
ni wa namna hiyo, unaweza kumbeba mgongoni au kwa jinsi yeyote ile
ambayo itakuruhusu kuendelea na shughuli zako nyingine.
5. Hitaji la mapumziko
Ni
rahisi kudhani kuwa mtoto atapata usingizi wakati wowote popote pale
alipo. Hata hivyo, kwa baadhi ya watoto, hali kama za ujio wa wageni,
kelele au hali ya fujo zinaweza kumfanya mtoto kusisimka na hivyo kuwa
vigumu kwake kutulia.
Watoto wachanga wanaweza kupata ugumu wa
kukabiliana na mambo ya kusisimua sana kwa mfano vitu kama taa, kelele,
au kubebwa kwa kupokezana kutoka kwa ndugu au mgeni mmoja mpaka mwingine
hasa wanapokuja kumtembelea mama.
Hali hii humfanya mtoto kushindwa
kustahamili na hivyo kuzidiwa na hayo yote.
Wazazi wengi wamegundua
kwamba watoto wao hulia zaidi kuliko kawaida wakati ndugu au jamaa
wakiwatembelea hususani nyakati za jioni. Kama hakuna sababu nyingine
maalum inayopelekea mtoto wako kulia, yawezekana basi kilio chake
kinasababishwa na uchovu.
Mzazi ama mlezi anashauriwa kumpeleka mtoto
sehemu tulivu iwe chumbani au sehemu nyingine ambapo patamwondolea hali
ya kusisimuliwa na hivyo kumfanya aweze kuacha kulia na kupata usingizi.
6. Hitaji la kitu cha kumfanya mtoto ajisikie vizuri
Iwapo
umemlisha mtoto wako na kuhakikisha kuwa yupo vizuri lakini akawa bado
anaendelea kulia, mzazi ama mlezi unaweza kuwa na hofu kuwa mtoto ni
mgonjwa au ana maumivu. Ni vigumu sana nyakati za mwanzo kwa mzazi
kutambua kuwa mtoto wake analia kwa sababu ya kutokuwa na furaha au kuna
kitu kinachomuumiza.
Mtoto ambaye ni mgonjwa mara nyingi hutoa sauti ya
kilio kilicho tofauti na sauti yake ya kawaida. Sauti hii inaweza kuwa
ya haraka zaidi au kali sana.
Vile vile kwa mtoto ambaye amezoea kulia
mara kwa mara, pindi anapoonesha hali ya utulivu isiyo ya kawaida
inaweza kuwa dalili ya kwamba ni mgonjwa. Jambo muhimu la kukumbuka ni
kwamba hakuna mtu anayemjua mtoto wako vizuri zaidi kuliko wewe.
Kwa
hiyo basi kama mzazi ama mlezi unahisi kwamba kuna kitu tofauti kwa
mtoto wako ni vyema ukaonana na wataalimu wa afya. Wataalamu wa afya
daima watayachunguza matatizo ya mtoto wako kwa umakini mkubwa na hivyo
kujua sababu ya mtoto kulia.
Mzazi ama mlezi unashauriwa kuonana na
daktari iwapo mtoto wako ana shida ya kupumua pindi anapolia, au kama
kulia kwa mtoto kunaambatana na kutapika, kuharisha ama kutopata choo.
7. Mtoto anahitaji kitu, lakini hujui ni nini
Wakati
mwingine unaweza kushindwa kufahamu ni nini kinachomsababishia mtoto
wako kulia. Wakati mwingine watoto wanakosa furaha.
Hali hii ya kukosa
furaha bila sababu inaweza kudumu dakika chache au saa kadhaa ambapo
mtoto huendelea tu kulia mara kwa mara.
Wakati mwingine baadhi ya watoto
hulia kwa muda mrefu huku wakirusha rusha miguu. Hii hali yaweza
kusababishwa na maumivu ayapatayo mtoto kwenye tumbo. Kwa kitaalamu hali
hii hujulikana kama colic.
Huwawia vigumu sana wazazi wengi kukabiliana
na mtoto ambaye ana colic. Hakuna tiba ya uchawi kwa colic, aidha ni
mara chache sana hali hii inadumu kwa zaidi ya miezi mitatu. Hata hivyo
ni vyema kupata ushauri wa daktari pindi unapohisi mtoto wako ana colic.
Je, nini cha kufanya mtoto anapolia?
Kuna
vitu ambavyo mzazi unaweza kufanya ili kumpa faraja mtoto wako pindi
anapolia. Yawezekana baadhi ya mambo yatakayoshauriwa hapa yasiwasaidie
watoto wote, hivyo basi mzazi ama mlezi ni vizuri ukamjua mtoto wako na
kufahamu kwa undani ni kitu gani hasa kinachoweza kusaidia kumtuliza.
1. Kumbeba mtoto
Watoto
wachanga huonyesha upendeleo fulani wa hisia, kama vile walivyokuwa
ndani ya tumbo, hivyo basi unaweza kujaribu kumvingirisha mtoto wako
katika blanketi au nguo zozote za kumbebea kama khanga au vitenge ili
kuona kama atapenda hali hiyo.
Watoto wengine hawapendi kuvingirishwa
kwenye blanketi na hupenda aina nyingine ya kupata faraja kama vile
kubebwa. Wapo wazazi wanaopenda kumbeba mtoto kiasi cha kumfanya mtoto
asikie mapigo ya moyo, kitendo ambacho humpa faraja sana mtoto.
2. Kumwimbia nyimbo au sauti za kumbembeleza
Akiwa
tumboni mwa mama, mara kwa mara mtoto alikuwa akisikia mapigo ya moyo
ya mama. Hali hii ndiyo sababu kubwa ya watoto wengi kupendelea kubebwa
na mama zao.
Hata hivyo kuna aina nyingine za sauti zinazoweza pia
kusaidia kumtuliza mtoto. Mzazi ama mlezi unaweza kujaribu kuweka muziki
wa taratibu au kumuimbia mtoto nyimbo za kubembeleza kwa sauti ya chini
sana.
Unashauriwa kutokuweka miziki ya haraka au yenye sauti kubwa kwa
sababu inaweza kumwondolea hali yake ya utulivu na hivyo kumfanya
ashindwe kuacha kulia.
3. Jaribu kumkanda au kumsugua taratibu (masaji)
Kumkanda
kanda au kumsugua mtoto taratibu mgongoni au tumboni kunaweza kumsaidia
sana kumfariji mtoto.
Iwapo inaonekana mtoto anapata tabu wakati wa
kubeua au kucheua, jaribu kumlisha akiwa wima zaidi na kila baada ya
kumlisha mweke juu ya bega lako na kumsugua taratibu mgongoni ili
kumsaidia atoe gesi kwa kubeua.
Baadhi ya watoto ambao wana “colic”
wakati mwingine hutulia hasa wanaposuguliwa taratibu tumboni na hii
huweza kuwafanya wajisikie vizuri kwa vile huihisi kwamba angalau mzazi
ama mlezi unajitahidi kufanya kitu fulani kusaidia kumwondolea shida
yake.
4. Mpatie kitu cha kunyonya
Kwa
baadhi ya watoto waliozaliwa, haja ya kunyonya ni kubwa sana na hivyo
kumpatia chuchu safi iliyotengenezwa kwa ajili hiyo au kidole kisafi cha
mama inaweza kuleta faraja kubwa kwao. Kunyonya kutamsababishia mapigo
ya moyo wake kuwa katika kiwango chake cha kawaida, kupumzisha tumbo
lake, na kutulia.
Ulezi
wa watoto wachanga ni kitu kigumu lakini ulezi wa mtoto ambaye hulia
mara kwa mara ni ngumu zaidi.
Kupata msaada na kuungwa mkono wakati
unapohitaji msaada ni muhimu zaidi.
Mzazi hana budi kufahamu kuwa kwa
jinsi siku zinavyopita, na kwa kadri mtoto anavyokua, mtoto anajifunza
njia mpya ya kuwa na uwezo wa kuwasilisha mahitaji yake na hivyo ni
muhimu mzazi naye kujifunza njia hizo ili kumuwezesha kumpatia mtoto
mahitaji yake anayohitaji kwa haraka na wakati unaostahili.
Imetumwa na Dr Paul J Mwanyika.
Read more: http://vitukovyamtaa.blogspot.com/.