Historia ya Rwanda ni ndefu iliyojaa misukosuko ya
kisiasa, kupinduana, vita na mauaji ya wenyewe kwa wenye
yaliyosababishwa na ubaguzi wa kikabila.
Rwanda imekuwa ikipita katika vipindi vigumu na
vya hatari. Vipindi hivi hufuatana na mauaji ya raia wa nchi hiyo, sio
tu kutokana na sababu za ukabila bali pia uongozi mbaya wa kisiasa.
Mwaka 1959, mtawala wa Kitutsi aliyekuwa
akiitawala nchi hiyo na kulalamikiwa kuwa utawala wake ulikuwa
ukiwaneemesha zaidi Watutsi walio wachache, uliangushwa na Wanyarwanda
wa Kabila la Kihutu.
Mabadiliko haya yalifuatiwa na mauaji ya takriban
Watutsi 150,000. Walioponea chupuchupu walikimbilia nchi mbalimbali
jirani na Rwanda.
Ni wakati huu wazazi wa Rais wa sasa wa Rwanda, Paul Kagame walikimbilia nchi jirani, Uganda yeye akiwa na umri wa miaka miwili.
Ni wakati huu wazazi wa Rais wa sasa wa Rwanda, Paul Kagame walikimbilia nchi jirani, Uganda yeye akiwa na umri wa miaka miwili.
Baada ya hapo, Wahutu wakaunda Chama cha PARMEHUTU, kikiongozwa na Gregoire Kayibanda, ambaye baadaye alikuwa Rais wa Rwanda.
Mtu angedhani wakati huo kuwa kwa sababu uongozi
wa nchi hiyo ulichukuliwa na kudhibitiwa na mtu kutoka kabila la Wahutu
waliokuwa asilimia 88 ya Wanyarwanda wakati ule, (Watutsi wakiwa
asilimia 11 na asilimia moja Watwa), kusingekuwa na chokochoko tena.
Utawala ungekuwa wa amani, wapi?
Mapinduzi ya kijeshi
Kinyume na matarajio, Julai 5, 1973 Serikali hii
nayo ilipinduliwa. Mapinduzi haya yalifanywa na jeshi la Wahutu
wakiongozwa na Meja Jenerali Juvenal Habyarimana, ambaye naye alikuwa
Mhutu.
Cha ajabu, licha ya tofauti hizo za kikabila,
mapinduzi hayo yalifanywa na Wahutu walio wengi wakishirikiana na
Watutsi wachache. Hii ilitokana na malalamiko kuwa Rais Kayibanda
alikuwa akiendesha nchi kama familia yake, akipitisha uamuzi bila
kushirikiana na viongozi wengine.
Baada ya mapinduzi hayo, kiongozi huyo mpya
alibadilisha mambo mengi ikiwa ni pamoja na kusambaratisha chama
kilichokuwa kikiongozwa na Kayibanda, PARMEHUTU, badala yake akaunda
Chama cha National Revolutionary Movement for Development MRND.
Miaka takriban 17 baadaye kutokana na kile
kilichoonekana kama utawala wa kikandamizaji, Watutsi waliokuwa nje ya
nchi walishirikiana na Wahutu wa ndani kuanza harakati za kuiangusha
Serikali ya Habyarimana.
Harakati hizi ndizo zilizomwingiza madarakani Rais wa sasa, Paul Kagame. Malalamiko kama yale yaliyosababisha mapinduzi dhidi ya mtangulizi wa Habyarimana yakajitokeza tena.
Mtu anayeangalia na kuchambua hali ya mambo ilivyo hivi sasa
hachelewi kung’amua kuwa hali kama ile iliyozikumba tawala za tangu
utawala wa kifalme wa Watutsi na tawala za Kihutu zinajitokeza tena.
Na hii inaifanya hali iwe tete kuliko wakati
wowote. Wengi wanaamini kama yatatokea mapigano au mabadiliko katika
Serikali ya Kigali pengine hali inaweza kuwa mbaya kuliko ilivyowahi
kushuhudiwa.
Hivi sasa Wanyarwanda hasa kutoka Kabila la
Kitutsi na ambao walikuwa bega kwa bega na Rais Kagame, baadhi ya wasomi
na maofisa wa juu kutoka jeshi la RPF wameikimbia Rwanda na tayari kuna
kampeni za chini kwa chini kutoka makabila yote mawili kuupinga utawala
wa Kagame.
Mbaya zaidi kuna kundi kubwa la vijana waliozaliwa
baada ya mauaji ya Rwanda. Hili ni kundi kubwa na mtu yeyote ambaye
amekuwa akitembelea kambi za wakimbizi kwa miaka mingi anaelewa
ninachoelezea hapa.
Mwaka 1997 nikiwa na waandishi wenzangu
tulitembelea kambi za wakimbizi kutoka Rwanda. Kulikuwa na idadi kubwa
ya watoto. Mmoja wetu alimuuliza mmoja wa wakimbizi kwa utani “nyinyi
mpo kwenye matatizo mbona mnazaa watoto wengi hivi, hamuoni ikiwa
mnajiongezea mizigo”?
“Hawa ndio watakuja kuikomboa Rwanda,” alijibu
kiongozi wa wakimbizi huku akipigiwa makofi na kundi la vijana waliokuwa
pembeni kusikiliza mahojiano, katika kambi ya Mbuba wilayani.
Nadharia hii imekuwa ikiendelea kwa miaka mingi.
Hata tulipotembelea kambi nyingine tukiandamana na Kamishna Mkuu wa
Shirika la Kuhudumia wakimbizi Ulimwenguni (UNHCR), Antonio Guateres
karibu waandishi wengi hawakuficha hisia zao za kushangazwa na kasi ya
kuzaana katika kambi za wakimbizi.
Fikiria kwa utaratibu huu watoto waliozaliwa tangu
mwaka 1994 ni watu wazima. Kama ni wanajeshi ni jeshi kubwa tena lenye
hamasa kubwa ya kurudi katika nchi yao Rwanda katika wakati ambapo
wanaona kikwazo ni Kagame na Serikali yake.
Hivi Kagame anajua kuwa kundi hili halibanwi na
tuhuma za mauaji ya halaiki ya Rwanda ya mwaka 1994? Hata wale
wanaotafutwa sio tena kitisho dhidi ya Serikali ya Kigali sababu ni
wazee sasa, wa kuogopa ni jeshi hili kubwa la vijana.
Hawa Kagame anawabana na sheria gani? Isipokuwa
kwamba wanajiandaa kupigana na Serikali yake kama yeye alivyofanya
kuipindua Serikali ya Habyarimana akitokea Uganda?
Kibaya zaidi ni kuwa makundi haya katika ukanda wa Maziwa Makuu, wana mawasiliano na kwa nyakati fulani yanasaidiana.
Ushauri wa Rais Kikwete
Ninaamini hiki ndicho kilichomsukuma Rais Kikwete kutoa ushauri
kwa marais hawa majirani zetu kuwa wasifanye kosa wazungumze na waasi.
Heri kupatana nao kwa sasa kuliko baadaye wakisharidhika kuwa
wamejiandaa vizuri na wakaanza mapigano rasmi.
Kila mwenye macho ya kuona mbali hachelewi
kumshauri Kagame chonde chonde ongea na waasi hawa, badala ya
kujiridhisha kuwa ni watuhumiwa wa mauaji ya halaiki, wakati wengine
mauaji hayo yalitokea wakiwa na umri wa miaka sita na kurudi chini, hawa
ni jeshi kubwa lenye uwezo wa muda mrefu wa kukaa msituni, ni hatari.
Yapo maswali kadhaa ya kujiuliza, hivi kwa nini
Rais Kagame hakioni hiki tunachokiona sisi? Kwa nini hakioni hiki
ambacho amekiona Rais mwenzake Kikwete?
Ninaamini Rais Kikwete hakukurupuka, ana vyombo
vya kiintelijensia vinavyomfahamisha kinachoendelea sio tu Tanzania,
lakini hata katika mapori makubwa na Misitu ya DRC.
Kagame anapaswa kusoma alama za nyakati,
asikimbilie kusema “watuache Rwanda tumalize matatizo yetu,” kwani baada
ya mauaji ya mwaka 1994 nchi hiyo ililaumu jumuia ya kimataifakuwa
haikuisaidia Rwanda kuepuka mauaji hayo.
Kama walivyosema Wahaya kuwa “ajuna akanyonyi
ajuna akakyahalala” maana ukitaka kumsaidia ndege msaidie akiwa bado ana
uwezo wake wa kupaa.
Badala yake ametoa lugha za matusi kashfa hadi
kutoa vitisho dhidi ya Tanzania, ati kwa ushauri aliopewa na Rais
Kikwete, kuwa azungumze na waasi wa Democratic Forces for The Liberation
of Rwanda (FDLR).
Kikwete alitoa ushauri huo kwenye Kamisheni ya
Ulinzi na Usalama ya Umoja wa Afrika wakati wa Mkutano wa wakuu wa nchi
za umoja huo uliofanyika mwanzoni mwa Juni mwaka huu, mjini Addis Ababa,
nchini Ethiopia.
Ushauri huo umegeuka mwiba na kitanzi dhidi ya
uhusiano uliokuwepo kati ya Tanzania na Rwanda, ingawa wengine tunajua
uhusiano huo haukuwa barabara tangu awali kwani kiongozi huyo wa Rwanda
mara kwa mara amekuwa akiisimanga Tanzania hata kabla ya ushauri huo
kutolewa.
Imekuwa kama vile jirani yetu huyu amepata turufu muhimu ya kuitishia Tanzania.
Imekuwa kama vile jirani yetu huyu amepata turufu muhimu ya kuitishia Tanzania.
Kinachoshuhudiwa sasa ni vita ya maneno baina ya
nchi hizi mbili yaani Tanzania na Rwanda.Vita ya maneno na majibizano ya
namna hii mataifa hujikuta katika vita kamili.
Kwa upande mwingine wengi walishangaa kwa nini Kagame aonekane kukerwa sana wakati ushauri huo haukumhusu yeye peke yake?
Wakati Paul Kagame akikabiliwa na kundi
linaloinyemelea nchi yake la FDLR, Joseph Kabila, wa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (DRC) anapambana na waasi wa sasa wa M23, na Rais
Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda akitishiwa na makundi mawili. Allied
Democratic Force (ADF) na Lord’s Resistance Army (LRA).
Hata hivyo, si Tanzania pekee ambayo imeona hatari inayoinyemelea Rwanda bali hata moja ya makanisa nchini Rwanda.
Hata hivyo, si Tanzania pekee ambayo imeona hatari inayoinyemelea Rwanda bali hata moja ya makanisa nchini Rwanda.
Kanisa hilo lilipeleka ujumbe hivi majuzi hadi Ikulu ya Kagame
likitabiri kuwa Rwanda inakabiliwa na matatizo makubwa na kuwa inaweza
tena kudidimia katika mgogoro mkubwa. Watumishi hao wa Mungu wameishia
kukamatwa na kuambiwa wanataka kuvuruga amani kuleta mgororo wa
kikabila.
Uasi zaidi
Kila kukicha wanajeshi wa Rwanda wanazidi
kulikimbia jeshi lao na nchi yao, siku zilizopita walikuwa wakikimbilia
Uganda siku hizi baada ya kuzidishwa ulinzi katika mpaka wa nchi hizo
mbili sasa wanakimbilia Afrika Kusini, nchi ambayo inajua kwa hakika
kitu gani kinaendelea nchini Rwanda. Inawapa hifadhi ya ukimbizi wa
kisiasa.
Miongoni mwao ni aliyekuwa Mkuu wa Usalama katika
Jeshi la RPF, Luteni Jenerali Faustin Kayumba Nyamwasa. Huyu alianza
kutofautiana mapema na Kagame, baadaye akamsogeza mbali na nchi hiyo.
Akamteua kuwa Balozi wa Rwanda nchini India.
Bado Kagame aliendelea kumwona ofisa huyo tishio,
hivyo akamtuhumu kuwa alihusika na milipuko ya mabomu February 2010
mjini Kigali. Wakati Kagame akiandaa utaratibu wa kumkamata habari
zikavuja, ofisa huyo akatoroka kutoka India hadi Afrika Kusini anapoishi
sasa.
Inafahamika kuwa maofisa wenye uwezo kama wa
Nyamwasa wakipata ushirikiano na wanamgambo wa Kihutu walio sehemu
mbalimbali nje ya Rwanda ni rahisi kuishambulia Rwanda, ndio maana
inasemekana wametumwa makachero kumuua Nyamwasa kule kule Afrika Kusini
lakini ‘wakachemka’ na kuishia kwenye mikono ya polisi ambapo walikiri
kutumwa na Serikali ya Kigali, kumuua Nyamwasa.
Mwezi Juni 2010, Kiongozi wa Timu ya mpira wa
miguu wa Rwanda Brigedia Jenerali Jean Bosco Kazura, alikwenda Afrika
Kusini kuangalia mashindano ya kombe la dunia, lakini aliporejea Rwanda
akakamatwa kwa tuhuma kuwa akiwa huko alifanya mawasiliano na Nyamwasa
na kwa maana hiyo akaingizwa katika kundi la wanaotaka kuiangusha
Serikali ya Kagame.
Jean-LĂ©onard Rugambage, mwandishi wa habari
ameuawa na makachero ikisemekana kuwa alikuwa akitumiwa na
Nyamwasa.
Maofisa wa Serikali ya Rwanda wanapotetea msimamo wa Rais Kagame wa kuikejeli Tanzania wanadai kilichomkasirisha bosi wao ni kushauriwa akae meza moja na wale anaowaona kama wauaji wa halaiki wa mwaka 1994, na kuwa ushauri huo ni sawa na kucheza juu ya makaburi ya Wanyarwanda waliopoteza maisha katika mauaji hayo.
Maofisa wa Serikali ya Rwanda wanapotetea msimamo wa Rais Kagame wa kuikejeli Tanzania wanadai kilichomkasirisha bosi wao ni kushauriwa akae meza moja na wale anaowaona kama wauaji wa halaiki wa mwaka 1994, na kuwa ushauri huo ni sawa na kucheza juu ya makaburi ya Wanyarwanda waliopoteza maisha katika mauaji hayo.
Hata kama ingekuwa hivyo, basi angewachukia waasi
wale lakini sio Tanzania kwa sababu baada ya mauaji ya Rwanda, iwe
Kagame au waasi wenyewe hakuna upande wowote uliowahi kuituhumu Tanzania
kuhusika kwa namna yoyote katika mauaji hayo, kwa sababu wanajua kuwa
nchi hii ilikuwa ikijua kila kilichokuwa kikiendelea na kikifanywa na
kila upande kabla na baada ya mauaji hayo.
Na hapo ndipo lilipo ‘fumbo la imani’ kwa nini Kagame amechukia sana kwa ushauri ule.
Sababu nyuma ya pazia
Udhaifu wa sababu ya chuki za Kagame unaashiria
kwamba kilichoikasirisha Rwanda ni uamuzi wa Tanzania kupeleka jeshi
lake lishiriki kulinda amani DRC, na sio ushauri ule.
Alijua kuwa sasa mengi yatafumuka, ambayo tayari Tanzania
inayafahamu ikichanganya na yale itakayoyagundua DRC.
Nina mifano mingi na ushahidi wa kimazingira hebu nitaje mmoja na kumalizia makala yangu.
Nina mifano mingi na ushahidi wa kimazingira hebu nitaje mmoja na kumalizia makala yangu.
Yaliyotokea 1994
Rwanda inajua, Kagame anajua, na dunia nzima
inajua kuwa mauaji ya kimbali ya Rwanda yalikolezwa zaidi ya kutunguliwa
ndege ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo wakati huo, Habyarimana.
Habyarimana na mwenzake wa Burundi, Syprian
Ntaryamirwa walikuwa wakitoka Arusha nchini Tanzania katika mojawapo ya
mikutano yenye lengo la kuangalia namna ya kugawana madaraka baina ya
Serikali ya Kigali ya wakati ule na kundi la waasi siku zile RPF.
Kikundi hiki cha RPF kikiwa na Watutsi wengi
kilikuwa kimeanzisha mapigano dhidi ya Serikali ya Habyarimana miaka
miwili kabla wakipigana kutokea nchini Uganda wakitaka Serikali itoe
nafasi kwa Watutsi karibu lakini tano waliokuwa wakiishi nje ya Rwanda.
Licha ya Serikali ya Habyarimana kusaini
makubaliano ya kuwaingiza waasi wa RPF katika Serikali ya Umoja wa
Kitaifa, Wahutu ambao ndio walio wengi walikuwa hawakubaliani na jambo
hili.Kwa hiyo, fikiria inakuja kufahamika kuwa Watutsi wale walioanzisha
mashambulizi kutokea nchini Uganda, wametungua ndege ya Rais wa kabila
lao na kumuua pamoja na makamanda wa ngazi za juu wa jeshi la Rwanda la
wakati ule.
Ndio maana baada ya kutunguliwa ndege hiyo Aprili
1994 mauaji ya kutisha yaliyodumu kwa siku mia moja yaliendelea na
kugharimu maisha ya Wanyarwanda laki nane, wengi wao wakiwa Watutsi na
Wahutu wenye msimamo wa wastani.
-Imeandikwa na Christopher Buke wa gazeti la mwananchi.
-Imeandikwa na Christopher Buke wa gazeti la mwananchi.