VIWANJA vya ndani (indoor ground) vya
‘Presidential Marathon 2015’ vina hekaheka nyingi sana. Kila mmoja yuko
bize kwenye kiwanja chake akijifua hofu ikiwa imetanda dhidi ya
wapinzania wake.
Safu ya wataka urais wa mwaka 2015 ni
ndefu pamoja na kwamba haiko hadharani.Nikiwa Mtanzania mnyonge lakini
kwa matakwa ya kizalendo naona nilete tafakari yangu kwa wanyonge
wenzangu tutafakari kwa pamoja. Lakini kwa madhumuni ya makala hii
nataka nimzungumzie mdau mmoja tu wa mbio hizi naye ni Edward Lowassa,
Waziri Mkuu aliyejiuzulu baada ya kuelemewa na kashfa ya Richmond
bungeni.
Wakati naandaa tafakari hii bado
naendelea kusoma kitabu maarufu kitwacho Defeating Dictators; Fighting
Tyranny in Africa and Around the World cha mwaka 2011 kilichoandikwa na
Prof. George B.N Ayittey raia wa Ghana aishiye nchini Marekani ambaye
pia ni mshauri wa Rais Obama juu ya masuala yahusuyo Africa.
Maudhui ya kitabu hicho yamejikita
katika ubovu wa serikali za kiimla, dhalimu ambazo ni hatari kwa
demokrasia na kwa sehemu kubwa zikiwa ni serikali za Kiafrika.
Anawatazama viongozi wa Afrika kama bandari yenye kushugulika na bidhaa
za hovyo hovyo tu.
Ukurasa wa nane anasema: “The continent
of Africa has the dubious distinction of harboring more dictators per
capita than any other region in the world.”
Anasema barani Afrika watu wanapigana
sana kuondoa uongozi mmoja madarakani unaoingia unakuwa na tabia zile
zile mfano pale anaposema: “We struggle very hard to remove one
cockroach from power and the next rat comes to the same thing.”
Profesa Ayittey anasema ili nchi za
ulimwengu wa tatu na hasa za Afrika zipate kuendelea ni lazima ziwe na
mageuzi ya kitaasisi (Institutional Reform). Anazitaja taasisi sita
muhimu katika mabadiliko ya kidemokrasia na kiuchumi kuwa ni;- uhuru wa
taasisi za habari/vyombo vya habari, uhuru wa mfumo wa kisheria, uhuru
wa tume za uchaguzi, uhuru katika Benki Kuu, mfumo huru na wenye
kuzingatia weledi wa vyombo vya ulinzi na usalama na uthabiti na weledi
wa asasi za kiraia.
Tunaweza kukubaliana kutokubaliana
kwamba mfumo wa ki-taasisi ndiyo nguzo kubwa ya kujenga utawala bora,
kujitegemea, demokrasia ya kweli na hatimaye uchumi imara wa taifa
husika.
Kwa bahati mbaya sana katika mataifa
mengi ya ulimwengu wa tatu Tanzania ikiwamo yamewekeza nguvu kubwa
katika MTU badala ya TAASISI.
Ni mfumo uliojikita katika akili zetu
(wapiga kura), umejikita kwa wasaka uongozi na jamii nzima ndiyo maana
baada ya viongozi wengi kuingia madarakani wamekuwa wakitengeneza hisia
kwa wananchi kwamba wao ndo nchi na nchi ndo wao hata ngazi ya majimbo,
jimbo ni yeye, yeye ni jimbo. Matokeo yake baadhi ya viongozi wamegeuka
kuwa majanga ya kitaifa.
Mwezi Machi, 1998 aliyekuwa Rais wa
Marekani wakati huo Bill Clinton akiwa ziarani barani Afrika aliwataja
Laurent Kabila wa DRC (marehemu), Yoweri Museveni wa Uganda, Paul Kagame
wa Rwanda, Melesi Zenawi wa Ethiopia (marehemu) na Isiah Afwerki wa
Eritrea kama viongozi shupavu wapya wa Bara la Afrika (New Leaders of
Africa).
Miezi miwli baadaye waliotiwa viongozi
wapya wa Bara la Afrika walianza kuchapana nchini Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na wengine wakizibadili katiba za nchi zao
kuwa viongozi wa milele madarakani. Miaka 10 baadae Marekani ikaona nchi
haziwezi kuendelea chini ya viongozi wa namna hii. Mwezi Julai, 2009
Rais Barack Obama akihutubia Bunge nchini Ghana alisema: “ Afrika
doesn’t need strongmen, it needs strong institutions.”
Kwamba Afrika inahitaji taasisi imara na si viongozi imara katika maana ya personalities na ubabe wa ki-dola.
Mhe, Lowassa ukimtazama vizuri katika
harakati zake za kutafuta mkataba wa kuingia katika Jengo Jeupe la
Magogoni anajenga zaidi u-mimi, uimara katika yeye, utegemezi wa dola
zaidi ya kutengeneza tasisi, jambo ambalo kwangu mimi hafai na hatufai
kwa masilahi mapana ya taifa letu hili tukufu.
Lowasa anatumia mbinu za kutaka kuingia Ikulu kwa kujipitisha katika makundi maalum kwa madai yasiyoingia akilini.
Anapita makanisani, misikitini na kwa vijana wasiokuwa na ajira kwa madai ya kutoa misaada kutoka kwa rafiki zake.
Anajua fika kwamba yeye ni sehemu ya tatizo la ajira kwa vijana. Nafasi alikuwa nayo, na uwezo alikuwa nao.
Hahitaji shahada ya Chuo Kikuu kujua
kwamba Lowassa anataka urais wa 2015 akiulizwa atakataa kwa hoja nyepesi
nyepesi. Lakini tuseme si dhambi kuutaka urais wa nchi hii kwasababu ni
haki ya kila mmoja kikatiba lakini hoja hapa ni pale mtu anapoutaka
kupitia mlango wa nyuma.
Wenye akili wanajiuliza kuna nini hadi mtu atembee gizani wakati fursa ya kutembea kwenye mwanga ipo?
Leo ziko tetesi za taarifa za utitiri wa
vyombo vya habari vyenye kumuunga mkono kimya kimya katika mbio zake
zake hizi. Upo utitiri wa wabunge na viongozi wengine ndani na nje ya
chama wenye harakati za kimya kimya za kumuunga mkono kwa methali na
nahau za hapa na pale zote zenye kumtweza na kumtukuza. Wapo viongozi wa
dini mbalimbali wanaomuunga mkono kimya kimya.
Wapo wahadhiri mbalimbali katika vyuo
kadhaa vya elimu ya juu hapa nchini vikiongozwa na baadhi ya wahadhiri
wa Chuo Kikuu cha Mt. Augustino cha Mwanza (SAUT) walio ‘bize’ eti
kumsafisha Lowassa. Wanamuandalia vijana na kukutana naye kwa ahadi ya
kuwatafutia ajira. Huu ni upuuzi na lazima tuukatae.
Nampinga sana Lowassa kwa hili kwa
sababu njia anayoitumia inaibua maswali mengi kuliko majibu. Hisia zetu
ni kwamba akipata nafasi hiyo ataturudisha kule kule kwenye “strongman”
badala ya “strong institution” kwanini asijitokeze hadharani akatueleza
ni kwa namna gani alichafuka, kwanini alichafuka, na anataka tumfanyie
nini ili asafishike na kwanini. Ili tumpime na tuamue.
Sisi sote ni mashahidi kwamba Lowassa ni mmoja wa wanamtandao waliomwingiza Rais Kikwete madarakani.
Wengine walikuwa Samuel Sitta, Rostam Aziz na Benard Membe. Kwanini asijitokeze hadharani akatwambia hivi mtandao wao bado upo?
Kama haupo ulikufa lini? Na kwanini? Sote tunajua hivi sasa wana uadui usioelezeka.
Wakati fulani Mwenyekiti wa CCM, Rais
Jakaya Kikwete, alinukuliwa na vyombo vya habari akisema watu hawa wana
uadui kiasi cha kutishiana kuwekeana sumu kwenye chai. Sasa kwakuwa
Lowassa anataka kuwa mrithi wa Rais Kikwete angetoka hadharani
akatwambia hivi aliyoyasema mwenyekiti ni ya kweli? Na kwanini ikawa
hivyo? Nini hatima yake?
Nasema hatufai mpaka hapo atakapoamua
kujitokeza hadharani ili tumuulize maswali na atujibu kuliko kujificha
nyuma ya misikiti na makanisa.
Anashindwa kuelewa sisi wanyonge hata
hiyo misaada haitufikii kamwe. Anashindwa kuelewa mfumo wa kidini
hauruhusu kuhoji matumizi ya pesa. Wanyonge hutumwelewi.
Wamachinga tunataka mfumo endelevu si pesa.
Tunataka elimu ya biashara si pesa.
Kwanini asijitokeze akatuambia ni kwa
namna gani ataweza kutengeneza taasisi imara ya urais anaoutaka ili sisi
wanyonge tupate kipato cha kutosha ili tuweze kuchangia ujenzi wa
makanisa na misikiti yetu badala ya yeye? Kwanini asitwambie jinsi ya
kuimarisha uchumi nchi ili tuweze kutengeza ajira zetu badala ya kusaka
za watu tena zenye manyanyaso?
Hivi mtu anayekutana na vijana wa vyuo
vikuu chini ya ukuwadi wa walimu wao akawaahidi kazi ilimradi wamuunge
mkono anafaa kwa taasisi ya urais? Hapa anachotaka kutwambia ni kwamba
ajira anazo kapuni ukimuunga mkono unapata.
Kila siku watu wanalia na serikali
inalia, lakini yeye mara kadhaa amenukuliwa akisema ukosefu wa ajira kwa
vijana ni bomu litakalo lipuka wakati wowote.
Kumbe yeye anazo ilimradi tu uwe upande wake, nadhani atakuwa ni mtu hatari sana kwa masilahi mapana ya taifa.
Lakini swali jingine kubwa ni kwanini hatuambii hao marafiki zake wanaompatia pesa ni kina nani?
Na wanampa kwa mkataba gani? Na kwanini
wanampa kwa wakati huu? Hivi hao ‘marafiki’ thawabu zao zinafika vizuri
wakipitia kwake? Au ni walemavu hawezi kutembea? Ni wazito sana hawawezi
kuingia kwenye magari na ndege? Wana ‘allergy’ na miale ya kamera za TV
ndiyo maana hatuwaoni? Au ni masharti ya kisangoma, wakionekana
hadharani pesa zinayeyuka mpaka zipite kwa mtu mwenye nywele nyeupe
nyeupe hivi? Maswali ni mengi kuliko majibu.
Tuna maswali ya kumuuliza kama pesa ni
za kwake alizipata wapi? Kumbukumbu zinatuonesha takriban maisha yake
yote amekuwa mtumishi wa chama na serikali, si vibaya akatwambia
alifanya fanyaje katika kupata fedha zote hizo.
Tuna tetesi nyingi za wizi wa pesa hapa nchini, sasa ili tusimuunganishe nazo ni vizuri akatoka mchana kweupe akasema.
Ni hitimishe kwa kusema taifa letu lina hali mbaya kiuchumi, kisiasa, kijamii na hata kiulinzi.
Tunapojadili mustakabali wa taifa letu
ni lazima kujadili tukiwa na mawazo mapana. Na wanaotaka kutuongoza ni
lazima nao wawe ni watu wenye mtazamo mpana wenye kujenga taasisi imara
badala ya kuwekeza katika nguvu za watu fulani fulani tu na kuacha umma.
Napendekeza na naomba wanyonge mniunge
mkono tuwe na kile kinachoitwa SOLIDARITY OF THE POOR, tuache mazoea,
katika hili mtu anayetaka kuwa kiongozi wetu na hasa katika ngazi ya
urais ajitokeze sasa aseme anataka kufanya nini, kwanini na kwa vipi?
Ili tumpime. Suala la uteuzi wake akiachie chama chake husika.
Nina imani mtu safi, mtu mwenye maono, mwenye hisia za dhati na umaskini wetu, chama chake hakitasita kumteua.
Kama hakitamteua basi sisi wanyonge
tutakiadhibu kwa kushindwa kuteua mtu wa watu. Njia za magendo katika
biashara ya urais tuseme NO.
Najua tupo wengi wenye hisia za
kimagendo katika biashara ya urais lakini kwa kuzingatia hali ya taifa
letu kwa sasa ‘tufute na tu-delete kabisa’. Sisi tunapita, taifa
litabaki.
Tukutane juma lijalo kama nitakuwa na
jicho na mkono ili nikutafakarishe kwanini makundi ndani ya CCM hayafai
kuongoza nchi. Mungu atusaidie.
Source: Dullonet
TOA MAONI YAKO HAPA