Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, Asangye Bangu
(kushoto) akizungumza na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi,
Phillipo Mulugo baada ya kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma
za Jamii, kilichofanyika katika Ofisi za Bunge jijini Dar es Salaam
jana. Picha na Salim Shao
Dar
es Salaam: Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Bodi ya Mikopo kwa
Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), zitawapa mikopo wanafunzi 1,107
kutoka katika bajeti zao, baada ya wanafunzi hao kulalamika kukosa
mikopo.Bodi kuanzia leo, itawaita wanafunzi hao wanaochukua masomo ya vipaumbele yakiwamo ya Hisabati na Sayansi, ili kujaza fomu upya.
Hata
hivyo kuna wanafunzi wengine waliokosa mikopo kutokana na kushindwa
kujaza fomu za kuomba, lakini masomo yao si ya kipaumbele na hivyo
kuachwa katika uamuzi huo. Takriban
wiki mbili zilizopita, zaidi ya wanafunzi 100 waliochaguliwa kujiunga
katika vyuo vikuu mbalimbali nchini kwa mwaka huu, waliandamana kwenda
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kwa lengo la kukutana na waziri
mwenye dhamana na wizara hiyo, Dk Shukuru Kawambwa, baada ya kukosa
mikopo.
Wanafunzi hao walisema wamenyimwa mikopo bila kupewa maelezo ya msingi licha ya kuilalamikia bodi ya mikopo. Uamuzi
huo wa jana, umekuja baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za
Jamii, kuzibana wizara na bodi, ikitaka kujua kilichosababisha wanafunzi
hao kukosa mikopo.
Naibu
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, alisema jana kuwa
baada ya kutafakari suala hilo, uamuzi umefikiwa kuwa wanafunzi hao
waitwe kujaza tena fomu za kuomba mikopo. “
Kilichoamuliwa ni kwamba wizara na bodi zitatakiwa kutafuta fedha
kwenye matumizi mengine, ili kuwapa mikopo wanafunzi hawa,” alisema. Naibu
Waziri huyo alisema, “Bodi itatakiwa kutafuta fedha hizi kutoka kwenye
matumizi mengine (OC), itabidi wajinyime wasisafiri na kuachana na
matumizi yasiyo ya lazima. Pia watumie fedha za marejesho ya mikopo
kugharimia wanafunzi hawa,” alisema Mulugo.
Wanafunzi
watakaofaidika na idadi yao kwenye mabano ni wale wanaochukua masomo ya
ualimu wa hisabati (20), ualimu sayansi (164), udaktari tiba (111) na
uhandisi umwagiliaji (7). Wengine ni ualimu (617), sayansi kilimo (20), uhandisi (70) na sayansi ya jamii (98). Mulugo
alisema jumla ya Sh3.1 bilioni zinahitajika kuwalipia wanafunzi hao na
kwamba bodi itatoa Sh 2 bilioni na wizara yake itatoa Sh1.1 bilioni.