Dar es Salaam. Wanasayansi nchini Marekani wamesema kuwa wamegundua aina
ya chanjo, ambayo mtu akipatiwa hataugua tena ugonjwa wa malaria maisha
yake yote.Ugunduzi huo ambao tayari umefanyiwa majaribio kwa watu kadhaa na
kufanya kazi kikamilifu ukiwa pia salama, utaandika historia ya kufuta
malaria na kuwa ugonjwa wa nadra kwa watu kuugua.Taarifa kwa gazeti hili iliyotolewa Alhamisi wiki hii na Taasisi ya
Marekani ya Kudhibiti Magonjwa ya Kuambukiza na Mzio (NIAID), inaeleza
kuwa chanjo hiyo iliyopewa jina, PfSPZ imeonyesha mafanikio hayo kwenye
hatua yake ya awali ya majaribio.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mtu akipatiwa chanjo hiyo mwili wake
unatengeneza chembe kinga ambazo zinakuwa na uwezo wa kuangamiza vimelea
wa malaria katika hatua yake ya mwanzo mara baada ya kuumwa na mbu.
Chanjo ya PfSPZ, inaelezewa kutengenezwa kwa vimelea dhaifu wa malaria ambao huhamasisha mwili kutengeneza askari wa kudumu.
Kumbukumbu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2010, zinaonyesha
kuwa zaidi ya watu 3.3 bilioni, ambao ni karibu sawa na nusu ya dunia
nzima wapo kwenye hatari ya kuugua ugonjwa wa malaria.
Katika kipindi cha mwaka huo, inaripotiwa kuwa watu 210 milioni
walibaini kuugua malaria, baada ya kupimwa hospitalini ambapo takriban
660,000 walipoteza maisha.
Asilimia 90 ya waliopoteza maisha walikuwa kutoka Bara la Afrika, licha
ya juhudi kubwa za kusambaza vyandarua vyenye dawa na dawa za tiba.
WHO inasema kuwa kuongezeka kwa mbinu za kuzuia na kutibu malaria katika
maeneo mbalimbali duniani kumesaidia kupunguza tatizo la malaria kwa
asilimia 25 na kwa asilimia 33 katika Bara la Afrika.
Imesema kuwa nchi nyingi za Afrika zina uwezo mdogo wa kifedha, hivyo
hutegemea mataifa tajiri kuzisaidia kwa kuwezesha kupatikana vifaa vya
kuzuia malaria na dawa za tiba za bei nafuu, hata kutolewa bure kwa
watoto na wajawazito.
Mwananchi