ZAIDI ya watu 10 ambao wanadaiwa kuwa ni majambazi, wakiwa na mapanga na
marungu, wamevamia kituo cha mafuta cha Derina Petrol Station,
kilichopo Kibaha Picha ya Ndege, mkoani Pwani na kupora Sh milioni 15 na
vinywaji mbalimbali vilivyokuwepo katika Super Market ya kituo hicho.
Majambazi hayo yanadaiwa kuvamia kituo hicho kinachomilikiwa na
David Mosha, saa saba usiku ambapo yalifanya fujo kwa kutumia silaha za
jadi, hali iliyowafanya wafanyakazi wakimbie.
Akithibitisha
kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei,
alisema majambazi hao walifika katika kituo hicho wakiwa na magari
mawili, moja ni Prado na jingine Saloon yenye rangi nyeupe, ambayo yote
yaliegeshwa karibu na pampu za kuwekea mafuta.
Alisema kuwa,
baada ya magari hayo kusimama, majambazi hao wakateremka na kumkamata
mfanyakazi wa zamu aitwaye Samson Rufunga (33) na mlinzi wa kituo hicho,
Mohamed Shaban (47).
Kamanda Matei alisema baada ya kukamilisha
kazi hiyo, majambazi hayo yaliwafunga kamba za miguu na mikono
wafanyakazi hao na hatimaye kuwafungia ndani ya chumba kimoja kilichopo
katika kituo hicho.
Watu wengine waliokamatwa ni pamoja na Frank
Nyamahaga (28), ambaye ni dereva mkazi wa Tabata, ambaye walimpora Sh
100,000 na funguo ya gari yake aina ya Scania iliyokuwa imeegeshwa
kituoni hapo.
Mwingine aliyekamatwa na kuporwa ni Isack Silinu
(25) ambaye alikuwa utingo wa Scania hiyo mkazi wa Ipogoro, Iringa,
ambaye naye aliporwa simu na fedha taslimu.
Wengine waliporwa
katika kituo hicho ni Issa Mohamed (25), mfanyabiashara mkazi wa Frelimo
Iringa, ambaye aliporwa simu ya Nokia yenye thamani ya Sh 75,000 na
pesa taslimu Sh 68,000, wote walikuwa wakisafiri katika lori.
Mbali
na hao, lakini Juma Selemani (30) ambaye ni dereva wa pikipiki mkazi wa
Mwanalugali Kibaha ambaye alikwenda kituoni hapo kwa ajili ya kununua
mafuta aliporwa pikipiki yake aina ya SANLG na fedha taslimu Sh 4,600.
Hata
hivyo katika tukio hilo hakuna mtu aliyejeruhiwa, lakini Jeshi la
Polisi mkoani Pwani linaendelea na jitihada za kuwasaka majambazi hao
ili waweze kutiwa nguvuni.
TOA MAONI YAKO HAPA