MTOTO aitwaye Mwajuma Haji (16) ambaye amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili anayesumbuliwa na ugonjwa wa kusinyaa kwa viungo yuko katika hali mbaya baada ya baadhi ya ndugu kudaiwa kutaka auawe ili kutoa uchuro katika familia.
Kwa mujibu wa mama mzazi wa mtoto huyo, Tatu Musa baadhi ya ndugu (siyo wote) wamekata tamaa ya kumuuguza mtoto huyo na kupendekeza heri mtoto huyo akatishwe maisha yake.
“Mwanangu haumwi wala hajawahi kuumwa ila ghafla alianza kusinyaa na kukosa nguvu, kinachoniuma baadhi ya ndugu zangu wamekata tamaa wanataka wamuue, waniachie mwanangu,” alisema mama huyo huku akilia mfululizo.
Mwandishi wetu amemshudia mtoto huyo akiwa amesinyaa viungo kiasi cha kutoweza kufanya kitu chochote zaidi ya kulala.
Mama mzazi wa mtoto huyo alisema kuwa alijifungua mtoto huyo akiwa na afya njema lakini alipofikisha umri wa miaka mitatu hali ikabadilika na viungo vyake kuanza kusinyaa.
Mama huyo amedai kwamba kutokana na hali hiyo hakuweza tena kufanya shuguli za kumwingizia kipato zaidi ya kukaa na mwanaye kijijini kwao, Kiamange, Bagamayo mkoani Pwani bila ya kupata matibabu ya uhakika.
Alisema kwamba maisha ya mtoto wake yameendelea kuwa mabaya bila ya kupata msaidizi kutokana kutengwa na baadhi ya ndugu zake waliokata tamaa ya kumuuguza.
Aidha, Mama Mwajuma amedai kwamba kuna wakati alikuwa akimfungia ndani mwanaye kuanzia asubuhi ili aende kulima na kupata chochote, lakini aliporudi nyumbani alimkuta katika hali mbaya sana.
Kutokana na mazingira kuwa magumu, mama huyo alidai kwamba hakuwa na msaidizi wa kuweza kumwachia mwanaye ili aweze kuhangaikia kipato.
Mbali na mtoto huyo, mama huyo alibahatika kupata mtoto mwingine ambaye sasa ana umri wa mwaka mmoja na nusu lakini baada ya kujifungua mwanaye mkubwa akatokwa na vidonda mgongoni.
Baada ya mtoto huyo kusumbuliwa na ugonjwa huo kwa muda mrefu alishauriwa kumpeleka Muhimbili na kumuacha mwanaye mdogo kwa majirani.
Baada ya muda alipata taarifa kwamba mtoto wake mdogo anaumwa, ikabidi akamchukue na kumleta Muhimbili ili aishi naye ingawaje hairuhusiwi kwa mtoto kuishi wodini.
“Nina wakati mgumu, kwa kuwa nina watoto wawili sina cha kufanya kwa kuwa huyu mwingine hajiwezi kwa chochote zaidi ya kumsaidia kwa kila kitu, mbaya zaidi ndugu wamenitenga,” alisema huku akibubujikwa machozi.