MCHUNGAJI Ambilikile Mwaisapila wa
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) amesema Mungu ameendelea
kujifunua kwake na kumuonyesha kuwa Tanzania itakuwa kioo cha Afrika na
baadaye kioo cha dunia.
Ametoa kauli hiyo jana asubuhi
(Jumanne, Septemba 24, 2013) mbele ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakati
akizungumza na wakazi wa kijiji cha Samunge, wilayani Ngorongoro mkoani
Arusha wakati msafara wa Waziri Mkuu uliposimama nyumbani kwake ili
kumsalimia akiwa njiani kurejea mjini Arusha.
Mchungaji Mstaafu Mwaisapila maarufu
kama Babu wa Samunge alisema kuna mambo mengi ambayo yameandikwa kwenye
Biblia lakini hayakutokea Israeli na sasa yatafanyika hapa Samunge.
“Mungu ametupenda sana, yanakuja mambo makubwa na wala hayako mbali.
Kama mimi ni mzee na nitayaona, kwa hiyo mtarajie kuwa hayako mbali
kutokea,” alisema huku akishangiliwa.
Alisema katika mafunuo aliyopewa na
Mungu ameonyeshwa kwamba watu wengi zaidi watafurika kijijini Samunge
kuliko ilivyokuwa hapo awali. Alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali
kwa misaada iliyotoa wakati wa ‘kugawa kikombe’ ikiwemo mahema, maji na
ulinzi.
Waziri Mkuu ambaye yuko mkoani Arusha
kwa ziara maalum ya kusikiliza matatizo ya ardhi yanayowakabili wakazi
wa wilaya ya Ngorongoro, katika tarafa za Ngorongoro, Loliondo na Sale
alisema anakubaliana na utabiri wa Mch. Mwaisapila kwani Tanzania
imejaliwa gesi nyingi na mafuta mengi ambavyo vitabadili sura ya Taifa
hili.
“Mungu ametupa gesi nyingi sana, katika
miaka miwili tutakuwa na umeme kila mahali. Tuna makaa ya mawe ambayo
ni nishati kubwa na sasa tuna fursa ya kupata nishati ya umeme kutoka
ardhini (geo-thermal) katika Ziwa Natron,” alisema.
Alisema Tanzania imekuwa kimbilio la kila mwekezaji na sababu kubwa ni amani na utulivu uliopo nchini.
Aliwaeleza wakazi wa Samunge kwamba
mapema mwakani mkandarasi wa barabara atakuwa katika eneo lao kwa ajili
ya ujenzi wa barabara ya lami ambapo awamu ya kwanza itaanzia Wasso hadi
Mto wa Mbu kupitia Samunge.
Akitoa ombi maalum kwa niaba ya vijana
mbele ya Waziri Mkuu, Bw. Elias Kalumbwa alisema wanaomba kuchimbiwa
bwawa ili waweze kujiajiri kupitia kilimo cha mbogamboga na matunda.
Bw. Kalumbwa ambaye amesomea masuala ya
wanyamapori alisema eneo la kuchimba bwawa lipo katika mto wa msimu
unaopita kijijini hapo. “Eneo la kuchimba bwawa lipo katika mto wetu,
vijana tunaweza kujiajiri endapo tutapata bwawa ili tufanye kilimo cha
umwagiliaji maji,” alisema huku akishangiliwa.
Naye Bibi Martha Sereri (70) alimweleza
Waziri Mkuu kwamba wanaomba jimbo la Ngorongoro ligawanywe kwa sababu
ni kubwa sana kiasi kwamba inamuwia vigumu mbunge wao kufika maeneo
yote. Aliomba pia wapatiwe walimu wa sayansi na hisabati kwa ajili ya
shule 10 za sekondari zilizopo kwenye tarafa yao.
Aliomba wapatiwe mikopo ya matreka ili
waweze kuongeza ukubwa wa mashamba yao. “Tunaomba mikopo ya matrekta na
plau, haya mashamba umeyaona njiani yamelimwa na Wakenya. Ukikodisha
trekta kila ekari unatozwa sh. 100,000/-. Je tutafika wapi? Mkitukopesha
matrekta mtakuwa mmetusaidia zaidi,” alisema.
Akijibu hoja hizo, Waziri Mkuu alisema
hoja zao ni za msingi na kwamba suala la vijana kupatiwa bwawa ni jambo
linalowezekana kupitia mipangpo ya maendeleo ya kilimo ya wilaya
(DADPS).
“Andaeni
andiko lenu, inabidi litoke kwa wananchi na siyo Serikalini. Mkituletea
ni jambo linalowezekana kwani liko ndani ya mipango ya wilaya.”
Akijibu hoja kuhusu ukubwa wa jimbo,
Waziri Mkuu aliwaambia wakazi hao kwamba inawezekana kuongeza jimbo
isiwe suluhisho la matatizo yao kwa sababu ya jiografia ya eneo lao.
“Kuongeza jimbo inaweza isiwe jibu
la kila kitu kwani matatizo mnayopata yanatokana na jiografia ya eneo
lenu, kutoka Ngorongoro, Loliondo hadi huku Sale. Mimi nadhani tuangalie
pia uwezekano wa kuwapa Halmashauri ili kusogeza huduma kwa wananchi.
Tutaangalia njia zote mbili na kuona ipi italeta majibu ya haraka kwenu,” alisema.