Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana,
Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa TMAA, Bruno Mteta, alisema madini hayo
yalikamatwa kwa kipindi cha kuanzia Septemba 2012 hadi Julai, 2013.
Mteta
alisema matukio ya utoroshwaji wa madini yamekuwa yakihusisha wageni
zaidi, huku akitaja madini yanayoongoza kutoroshwa kwenda nje ni
Tanzanite (vito), Amber, Green Gunnet, Soil and gold, Red gold moon
stone na Green Tomalin.
Mteta alisema biashara ya kusafirisha
madini nje ya nchi kwa njia za magendo, hivi sasa imeshamiri nchini na
kuifananisha na biashara haramu ya usafirishaji wa dawa za kulevya.
“Biashara hii hufanywa sana na raia wa nje, hatukatai watu wasifanye biashara ya madini, lakini wafuate utaratibu unaokubalika.
“Zipo
kesi zinaendelea mahakamani na kesi nyingine zipo mikononi mwa polisi
kwa uchunguzi, lakini zipo kesi tatu tayari hukumu imetolewa na madini
kutaifishwa,” alisema Mteta.
Mteta alisema Agosti 20, mwaka huu,
raia mmoja wa kigeni (hakumtaja jina wala uraia), alikamatwa Uwanja wa
Ndege wa Julius Nyerere akiwa na aina mbali mbali za madini yenye
thamani ya Sh. milioni 25.32.
Mteta alisema siku hiyo hiyo, TMAA
kwa kushirikiana na polisi walimkamata raia mwingine wa kigeni katika
makazi yake, Jangwani Beach, akiwa na madini ya vito vya thamani.
“Uthaminishaji
wa madini hayo unaendelea, japokuwa yanaonekana kuwa na thamani kubwa
sana, mtuhumiwa anaendelea kushikiliwa na polisi kwa uchunguzi zaidi,”
alisema.
Alisema TMAA ipo katika hatua za mwisho kuweka mtambo wa
kisasa katika viwanja vyote vya ndege, utakaosaidia kubaini watu
wanaotorosha madini kwenda nje ya nchi.
“Ni vigumu sana kubaini
mtu akiwa amebeba madini, sababu hakuna sauti inayotoka pale mtuhumiwa
anapopita kwenye mashine za usalama kwenye viwanja vya ndege,
ikilinganishwa na dawa za kulevya au kitu cha hatari,” alisema.