Serikali imetangaza majina ya wanafunzi 18,754 waliochaguliwa
kujiunga na vyuo vya ualimu vilivyo chini yake ikiwa ni ongezeko la
wanafunzi 1,659 ikilinganishwa na 17,095 waliochaguliwa mwaka jana.
Kati ya wanafunzi hao, 11,806 wamechaguliwa kusomea ngazi ya cheti (Grade A) na 6,948 watasoma katika ngazi ya stashahada.
Wanafunzi 363 wamechaguliwa kusoma elimu maalumu kwa ngazi ya cheti huku 57 wakisoma elimu hiyo kwa ngazi ya stashahada.
Akizungumza na mwandishi wetu jana, Msemaji wa Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi, Ntambi Bunyazu alisema wanafunzi wanatakiwa kuripoti
kwenye vyuo walivyopangiwa kuanzia Agosti 15, mwaka huu.
“Usajili utafungwa Agosti 25 saa 12:00 jioni, ‘Joining instructions’
(fomu ya maelekezo ya kujiunga) zitatumwa kwa wahusika kupitia anuani
zao.... fomu hizi pia zinapatikana kwenye tovuti ya Wizara ya Elimu na
mafunzo ya Ufundi,” alisema.
Taarifa ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iliyotolewa baadaye
jana ilisema kuwa wanafunzi waliochaguliwa wanatakiwa kufika vyuoni
wakiwa na vyeti halisi vya kidato cha nne na cha sita vinavyotolewa na
Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) , ada ya muhula wa kwanza
Sh100,000 au Sh200,000 kwa mwaka.
Wanatakiwa kuwa na “Sare ya chuo kulingana na maelekezo ya chuo
husika, fedha za tahadhari chuoni na matumizi binafsi,” inasema taarifa
hiyo.
Taarifa hiyo inaeleza pia kuwa wakuu wa vyuo wanatakiwa kuhakikisha
wanafunzi wanaosajiliwa ni wale waliopo kwenye orodha iliyotolewa na
wizara na si vinginevyo.
Wengi wa wanafunzi hawa ni wale waliohitimu kidato cha nne mwaka 2012
na kidato cha sita mwaka huu. Kwa upande wa wale wa kidato cha nne,
matokeo yaliyotangazwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
yalionyesha kuwa watahiniwa 159,609 wa shule walifaulu kwa daraja la
kwanza mpaka la nne.
Inaonyesha pia kuwa kwa upande wa Tanzania Bara, wanafunzi 34,599
walifaulu kwa daraja la kwanza mpaka la tatu na kati yake waliochaguliwa
kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya ufundi walikuwa ni 34,213.
Kwa upande wa matokeo ya kidato cha sita mwaka huu, watahiniwa
waliofaulu mtihani huo walikuwa ni 44,366 kati yao 40,242 wakiwa ni wa
shule. Matokeo hayo yanaonyesha pia kuwa, watahiniwa 35,880 ndiyo
waliofaulu kwa daraja la kwanza mpaka la tatu.
Kwa mujibu wa Kitabu cha Takwimu cha Wizara ya Elimu (Best), mwaka
2012 wanafunzi 17,095 walichaguliwa kujiunga na vyuo mbalimbali vya
ualimu nchini.
Kutokana na takwimu hizo, kuna uwezekano mkubwa kwamba wanaokwenda
kusoma ngazi ya cheti wanatoka kwenye kundi la wanafunzi waliopata
daraja la nne.
Wanafunzi waliopata daraja la nne kwenye mtihani wa kidato cha nne mwaka jana ni 124,260.
Baada ya kutangaza majina ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na
kidato cha tano pamoja na vyuo vya ufundi, Naibu Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo aliliambia gazeti hili kuwa wanafunzi
waliopata daraja la nne katika kiwango cha alama 27 watachaguliwa
kujiunga na vyuo vya ualimu endapo wataomba.
“Vigezo vya kujiunga na kidato cha tano na vile vya vyuo vya ualimu
ni tofauti. Kidato cha tano mwisho anatakiwa mtu mwenye alama 25 na
masomo yake matatu yawe sawa, ualimu ni alama 27.
“Mwanzoni walikuwa wanakwenda wenye alama 28, lakini mwaka jana
tukasema hapana, iwe alama 27 na tutachukua kuanzia waliomaliza shule
mwaka 2008 kama wataomba, kwa sasa hivi watu wanaendelea na kazi ya
kuwachagua,” alisema Mulugo.
Kwa muda mrefu, wadau wa elimu wamekuwa wakipiga kelele kuhusu
wanafunzi wanaochaguliwa kusomea ualimu nchini wakitaka nafasi hiyo
ichukuliwe na wale wanaofanya vizuri kwenye masomo yao.