Wafuasi wa aliyekuwa rais Mohammed Morsi
Wafuasi wa Rais wa Misri aliyeondolewa madarakani Mohamed Morsi --
wamekataa wito uliotolewa na wizara ya mambo ya ndani kumaliza
maandamano yao katika medani mbili kubwa za mjini Cairo.
Msemaji wao Alaa Mostafa amesema maandamano yao yataendelea.
Wizara iliwataka waandamanaji kuondoka na kuwapa fursa ya kuwalinda
wakati wakiondoka na ahadi ya kutowapeleka mahakamani iwapo watatii
maelekezo ya wizara hiyo.
Jumatano serikali inayoungwa mkono na jeshi nchini humo iliamuru polisi
kuwatawanya waandamanaji walioweka kambi katika midani hizo.
Bw. Morsi Rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia aliondolewa na jeshi
mwezi mmoja uliopita. Marekani imeitaka Misri kuheshimu uhuru wa
kukutana ikiwemo kuweka kambi katika maeneo ya mikusanyiko.