Home » » HESABU MAKOSA HAYA 7, HAKIKISHA HUYAFANYI KATIKA UHUSIANO WAKO-

HESABU MAKOSA HAYA 7, HAKIKISHA HUYAFANYI KATIKA UHUSIANO WAKO-

BADO tunaendelea na mada yetu tuliyoianza wiki nne zilizopita juu ya makosa ambayo hutakiwi kuyafanya unapokuwa kwenye uhusiani.
Pointi hapa ni kuwa mwanzo kabisa wa uhusiano, yapo mambo mengi ambayo kila mmoja hujitahidi kuyazungumza. Hiyo huitwa kujiweka wazi lakini imethibitika kitaalam kwamba maelezo ambayo hutolewa ni asilimia 40 tu, zilizobaki hufichwa. Asilimia 60 zilizobaki utazifichua kwa kusoma alama muhimu.

Nyongeza ni kwamba mara nyingi wengi hujitahidi kusema uongo mwanzoni mwa uhusiano. Hata kama mtu anapenda lakini hudanganya hili na lile pengine kwa hofu, tahadhari au kama pointi ya kushinda penzi. Mantiki hapa ni kukutaka uwe makini na umsome mwenzako kwa undani kabisa.
Katika kipengele cha kusoma alama muhimu, kuna vitu vya msingi vya kuzingatia ambavyo ni hivi vifuatavyo;
1) Jamii: Mwenzi wako anasimama vipi na jamii yake? Usiingie kichwakichwa kwenye mapenzi na mtu ambaye hata jamii yake inamuona ni tatizo. Vilevile, yule ambaye ni muoga inabidi uanze kumtilia wasiwasi mapema. Ni kwa ajili ya maisha yako, hivyo ni vema kuchangamka.
Hutakiwi kugundua muda umeshapita kuwa mwenzi ana tabia usizozipenda. Mapema msome na umuelewe. Chunguza msimamo wake kwenye jamii, anavyojiamini. Je, anaonesha kuwa na dira ya maisha? Kama hana uelekeo, unatakiwa kuachana naye haraka.
2) Hisia: Zisome hisia zake, je, ni mtu anayejali? Unatakiwa kujua kama hisia zake zipo karibu kwa kiasi gani. Atakapotakiwa kukutimizia haki yako ya faragha, atakuwa tayari kwa wakati? Ni aibu mmeshakuwa na uhusiano kwa muda mrefu ndiyo unaanza kulalamika kwamba mwenzi wako hakutimizii huduma ya uwanja wa wawili.
Lingine kwenye hisia, unatakiwa ujifunze kujua kama mwenzi wako ni mtu wa kulipuka au kinyume chake. Inawezekana ni kweli mwenzi wako anakupenda lakini akawa ni mtu wa jazba, tatizo dogo ‘anapaniki’ utadhani nyoka aina ya swila, kakanyagwa mkia. Mjue halafu umpime, je, unaweza kumvumilia? Jiridhishe mara mbili, vinginevyo bwaga manyanga.
3) Muonekano: Ni kipengele kidogo muhimu ndani ya kifungu cha kushindwa kusoma alama kama sehemu mojawapo inayowafanya wengi kufanya makosa kwenye uhusiano. Muonekano si suala la baadaye, inatakiwa mapema sana umtathmini halafu ujiridhishe kama anakufaa au kinyume chake.
Ni aibu umeshaingia kwenye uhusiano, halafu baadaye unamsaliti mwenzi wako na kuanza kuwatolea macho wale ambao unaona ni wazuri zaidi. Hakikisha kwamba mwanzo kabisa kwenye uhusiano wako, unajiridhisha kuwa anao mvuto unaokutosha. Kama hakuvutii achana naye mapema, usimpotezee muda wako.
Muda wako pia ni mali, kwa hiyo hilo pia litazame kwa umakini kwa sababu inawezekana ukachukulia ni jambo dogo leo, ukaanza naye uhusiano kwa kujifurahisha lakini mbele ya safari utakapotaka kuamua, ikakugharimu kwa maana pengine wakati wewe unawaza kutoka, mwenzako ndiyo kwanza anaongeza gia.
4) Kipimo cha mapenzi: Hiki ni kipengele nyeti. Kina maana kubwa, kwa hiyo hupaswi kudanganyika kwa namna yoyote ile. Hakikisha upendo wake kwako upo wazi. Wengi hushindwa kulifanyia kazi mapema, matokeo yake hubaki wakijuta baadaye. Chukua angalizo hili, kwa hiyo kama haoneshi upendo wa kweli, ni vema umuache aende.
Je, anaonesha yupo tayari kwa ujenzi wa uhusiano imara? Yupo wazi kwako na anapenda kila mtu ajue kwamba yeye ni wako? Alama hizo ndizo ambazo zinaweza kukupa muongozo unaojitosheleza. Kama upendo wake ni wa wasiwasi, nawe mkatae haraka. Wekeza upendo kwenye upendo, vinginevyo wewe utampenda lakini mwenzako atakudharau.

KUAMUA UHUSIKA WAKE KWENYE UHUSIANO
Ni rahisi kuamua jinsi ambavyo wewe unavyoweza kuhusika kwenye uhusiano wako lakini si yeye. Kufanya hivyo ni sawa na kuingia kwenye moyo wa mwingine, kitu ambacho hakiwezekani hata kiduchu. Kaa ukijua kwamba nafsi ya kwanza itabaki kuwa ya kwanza na ya pili itaendelea kusimama katika uhalisia wake.
Maisha ni kama picha ambayo unaijenga kwenye fikra zako. Endapo utawaza mema na kutamani kumfanyia mwenzi wako vitu vizuri, ni rahisi kutekeleza. Utakosea mno, kama utakuwa unasumbuliwa na mawazo kwamba unachokitenda, mpenzi wako naye atakaa na kufikiria kisha akutendee kama unavyomfanyia.

Itaendelea wiki ijayo.
GPL

TOA MAONI YAKO HAPA

 
Support : Copyright © 2011. HABARILINE - All Rights Reserved