Jimama mwenye hadhi yake ambaye ni mke wa mtu aliyetajwa kwa jina moja
la Mary au Mama Gilo, mkazi wa Sinza jijini Dar amekula kichapo cha
kutisha almanusra apoteze uhai baada ya kunaswa akiiba nguo kwa ajili ya
Sikukuu ya Eid El Fitr.
Tukio hilo la aibu lililoshuhudiwa na mwandishi wetu lilijiri katika
moja ya maduka makubwa ya nguo Kariakoo, Dar mwishoni mwa wiki
iliyopita.
Mama Gilo ambaye anafahamika Kariakoo na Sinza, alinaswa akiiba nguo za sikukuu ikiwa ni pamoja na ‘madira’ ya kumalizia mfungo.
Katika tukio hilo lililokusanya kadamnasi, mwanamke huyo alipigwa chabo
kwenye duka la mfanyabiashara Rehema Kessy ambapo alidai kuwa alifika
Kariakoo kwa lengo la kununua madira lakini alijikuta akiingiwa na tamaa
ya kuiba ndipo akanaswa.
Awali, kabla ya kuwekwa chini ya ulinzi na raia waliokuwa na hasira
kali, mwanamke huyo alidaiwa kukwapua mkoba wa mwanamke mwenzake na
kujichomeka kwenye maduka kumkwepa aliyemuibia ‘pimajoto’ lake
linalodaiwa kuwa na vitu ndani yake.
Baada ya kutiwa mikononi ndipo watu waliokusanyika wakauliza: “Na tumfanye nini mwanamke huyu?”
Watu wakapaza sauti wakisema: “Kwa utaratibu wetu hapa Kariakoo kwa
mwizi yeyote, hakuna adhabu nyingine zaidi ya kusulubiwa hadharani.”
Ndipo ikaamriwa asulubiwe kwa kupewa bonge la kipigo na kufanya watu
kutanda kwenye duka hilo kwa muda wa saa nzima bila kutoka, wakitaka
aachiwe ili wamalize kazi yao ya kumtoa roho kama adhabu ya mwizi
anapokamatwa Kariakoo.
Katika kusulubiwa huko, Mary alikuwa akilia kwa uchungu mkubwa akisema:
“Naombeni mnisamehe, nimekuwa nanyi siku zote tukifanya biashara ya
madira, leo mnaniua? Naombeni mumpigie simu mume wangu baba Gilo aje
anisaidie.”
Alipoambiwa akiri kuhusika na upotevu wa madira madukani katika
mazingira ya kutatanisha kisha atasamehewa, alisema: “Ni kweli nakiri
mbele yenu na Mungu awe shahidi, nimekuwa nikifanya kazi hii (kuiba
madira) pamoja na wanawake wenzangu watatu lakini wamenikimbia.”
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, si mara ya kwanza kwa Mary
kukamatwa kwa wizi kwani mwanzo aliwahi kudakwa, akavuliwa mpaka nguo
lakini amerudia tena kazi hiyo.
Ili kumnusuru, mmoja wa wasamaria wema aliyehisi uchungu kwa kuwa
mwanamke huyo alikuwa akilalamika kuwa anakata roho, aliwapigia simu
polisi wa Kituo cha Msimbazi, Kariakoo na kuwaambia: “Wahini mara moja
hapa jirani na shimoni. Kuna mwanamke mwenye hatia ya wizi anasulubiwa.
Njooni mumuokoe.”
Ndani ya ‘dakika sifuri’ polisi na ulinzi shirikishi walifika eneo la
tukio lakini walipomuona mtu waliyekuja kumuokoa akiwa ameshalegezwa ,
ikabidi waagize tolori la kumbebea.
Tolori liliposogezwa jirani na mwanamke huyo alipakizwa na kumkimbiza
huku wananchi wakimsindikiza kwa kumzomea wakati wengine wakitaka
kumponda na mawe hadi afe.
Mwisho wa yote mwanamke huyo alikwenda kubwaga kituoni Msimbazi akiwa
amepoteza fahamu kisha kufanyiwa utaratibu wa matibabu kabla ya kesi .
Credit; GPL