
Hata hivyo, kwa wale wanawake wachache ambao husuasua kuolewa hizi ni
baadhi ya sababu zinazopelekea kusuasua huko. (Izingatiwe hii ni kwa
wanawake ambao hawajawahi kuolewa kabisa)
Vigezo vilivyopitiliza viwango (hasa kwa muonekano)
Wanawake wengi hasa wa umri mdogo (lakini unatosha kuolewa) hutumia muda
mwingi katika kuchagua aina ya mwanaume ambaye angependa awe mume wake.
Wanawake hawa hujiamini zaidi na kusimamia sifa zile ambazo huamini ni
muhimu mwanaume wa kumuoa awe nazo. Vigezo hivyo huwa hata kwa misingi
ya muonekano wa mwanaume huyo – kuna wale ambao hutaka mwanaume huyo wa
kumuoa awe na sifa kama vile, mrefu, aliyejazia kifua, mtanashati, sauti
nzuri n.k. Inaweza kuwa kama mzaha na ikaonekana ni kipengele kidogo
sana lakini bado kuna wale ambao anaweza kuwa tayari kuolewa ila hataki
sababu tu huyo mwanaume hafananii vile ambavyo yeye anataka mumewe awe.
Kutaka mwanaume tajiri
Kuna wanawake ambao tayari wameshajiwekea akilini kuwa hatakubali
kuolewa na mwanaume yeyote yule ambaye hana pesa nyingi. Yupo tayari
kuolewa ila si kwa mwanaume mwenye uwezo wa kawaida – hata ikitokea
mwanaume ana uwezo kidogo wa kuweza kujitosheleza, yeye bado huona huyo
mwanaume hamfai hadi pale tu atakapo pata yule ambaye anahisi ataishi
maisha ya kifahari. Hivyo hukazana kusubiri na kujitahidi kuwinda aina
ya mwanaume ambaye atakuwa na uwezo mkubwa, bila kujalisha kama huyo
mwanaume kampita sana umri.
Kutompata Mwanaume Ampendae
Hili ni kama tu vile ilivyo kwa wanaume ambao huamini ndoa haiwezekani
na haifai bali tu hadi pale umpatapo yule ambaye unampenda na unaamini
anakupenda pia. Wengi katika kundi hili huamini kuwa mafanikio ya ndoa
kigezo kikubwa ni kupendana tu na mengine hufuata kwenye sababu ya
upendo. Kuna wanawake vigezo vya mwanamme awe vipi havina umuhimu kabisa
katika kutaka kuamua kuolewa. Yeye kikubwa anataka ampate mume ambaye
atampenda kwa dhati na huku akiwa na matumaini kuwa huyo mume atampenda
na yeye pia kwa dhati. Huyu mwanamke anaamini msingi bora wa ndoa ni
mapenzi ya dhati kati ya yeye na mmewe basi! Hana haraka hadi pale
atakapompata mwanaume akampenda ndipo atakapokuwa tayari kuolewa.
Kuchagua mno Wanaume wa Kumuoa
Kuna wale wachache ambao akili hubadilika kama kinyonga; wasioridhika
wala kujitambua ni nini wanataka ama mwanaume wa aina ipi wanataka.
Akija wa mwenye uwezo atasema nataka wa kuchuma nae, akija asiye na
uwezo atatoa sababu tu hata kama kumlaumu kuwa inaonyesha hajitumi
kutafuta maendeleo. Akija wa kabila hii, atasema hapana hao wana tabia
hii mimi siitaki! Yaani kwa ufupi ni mtu asiyeisha kutoa kasoro za wale
ambao wanajitokeza kutaka kumuoa. Hatimaye inaweza tokea muda wa kuolewa
ukapita na akaishia kupunguza uchunguzaji lakini ikiwa hata wanaume wa
umri wa kufaa kumuoa kutokuwepo tena katika soko.
Kujiona ni mzuri sana
Kuna wanawake ambao ni kweli Mwenyezi Mungu kawajaalia uzuri hasa (uzuri
wa muonekano), anakuwa ni mzuri kiasi kwamba wake kwa waume wote
wanamkubali kwa uzuri huo na hata wote kumtamani. Hata hivyo hapo hapo
kuna wale ambao huwa ni wazuri kawaida – ila kwa mtazamo wake hujiona ni
mzuri mno hakuna mfano kama yeye; kitendo ambacho kwa wachache kwenye
kundi hili hufanya kujiona yeye ni yeye na kuwa kwa yeyote kuwa na yeye
huyo mtu anatakiwa atambue kuwa ana bahati sana. Kitendo hiki hukuza
nyodo za hali ya juu ya mwanamke mwenye mtazamo huu, kiasi kwamba
wanapojitokeza wanaume kutaka kuoa – anaweza onyesha tabia kama maringo,
dharau na kiburi.
Kujiona ana Umri mdogo
Binti yeyote wa miaka 18 na kuendelea anaruhusiwa kuolewa endapo tu
karidhia kuolewa. Wanawake wametofautiana mipangilio yao ya kimaisha,
kuna wale akiwa katika umri wa kuolewa hutamani sana kuolewa na kuna
wale ambao hupenda kuolewa wakiwa wakubwa zaidi. Katika kundi hili umri
kuwa mdogo hutegemeana, kuna mwingine anakuwa na umri wa miaka 25 na
bado akajiona mdogo na hali kuna mwingine anakuwa na miaka 20 na
akajiona ni mkubwa na anafaa kuolewa. Hii pia ni kwa wanawake wale ambao
huwa na malengo ya kutotaka kuharakisha katika ndoa. Anapokuwa na umri
ambao anaweza kuolewa lakini yeye hayupo tayari kwa muda huo, huwa ni
kikwazo kwake kuingia katika ndoa.
Maradhi hasa UKIMWI
Hili kama lilivyo kwa wanaume - Pamoja na kuhamasishwa kwingi na
wataalamu wa maradhi ya HIV/AIDS kuwa mtu hata ukiwa umeathirika unaweza
kuwa na mahusiano na hata kuoa na kuwa na watoto; bado haisaidii sana
kwa vijana wanaojitambua kuwa ni waathirika wakiwa bado ni wadogo,
hawajaoa/olewa ama kuwahi kuwa na mtoto. Wengi sana hukata tamaa na
huona ni kheri kubaki walivyo kuliko kuingia katika ndoa, hasa tokana na
imani kuwa wanawake wakizaa wakati ni waathirika; afya hudhoofika
zaidi.
Kutaka maisha ya Tamthilia (Ndoa za kuishi kwa furaha milele)
Kutokana na kukua kwa idadi ya tamthilia nyingi ambazo huonyesha maisha
ya kimagharibi zaidi; kumekuwa na dhana kwa baadhi ya wanawake kutaka
hayo maisha ya tamthilia yawe na kwao pia. Hilo linafanya vigezo ambavyo
mwanamke huyo anatumia kuchagua ama kukubali mwanaume kumuoa kutotimiza
yale ambayo yeye binafsi anatarajia. Wengi hushindwa kutambua kuwa
hakuna maisha ya furaha milele, na hasa kuwa maisha ya maigizo yapaswa
kuchanganya na zako kuweza kufanya maamuzi ya kipi kiigwe na kipi
kiachwe kama kilivyo.
Kuona taasisi ya Ndoa kama Utumwa
Mtazamo huu kwa wanawake wenye msimamo huu, huchangiwa na baadhi kama haya:
- Usomi: Aina ya usomi ambao hupelekea kwa baadhi kuwa na tafsiri tofauti juu ya ndoa, haki, majukumu na mengine mengi.
- Kushuhudia ndoa mbovu: Hii inaweza kuwa ya wazazi/walezi wake wenyewe
(pengine mama aliteswa sana), na hata ndugu wa karibu kama vile
kushuhudia kila ndoa ya ndugu yake anayoijua mwanamke huishi kwa mateso,
manyanyaso na maisha ya taabu na kuonewa.
- Kuwa na uwezo sana wa kujitosheleza ambao unaweza kumtimizia na
kufanya lolote lile ambalo anataka katika maisha. Kwake kuwa na mwanaume
kama mume kwake anaona kama ni utumwa.
Kutokuwa kabisa na mshipa wa hisia za kufanya mapenzi
Kuna wanawake wale wachache waliozaliwa hivyo. Hawana hisia yoyote ile
ya kimwili ya kuweza kupata hisia za kuweza kujisikia ama kutamani
kufanya mapenzi. Wengi wa aina hii ya wanawake huwa ni waoga sana wa
kuwa karibu na mwanaume, na kwa wale ambao wamewahi hata jaribu baadhi
huona kama kitendo cha ndoa ni kero, unyanyasaji na uchafu. Hivyo wazo
la kuwa akiolewa anatarajia kufanya kitendo cha ndoa mara kwa mara
kinamvunja kabisa hamu ya kutaka kuolewa.