Inauma sana! Mtoto Neema Nyamuhanga mwenye umri wa miaka mitano, mkazi wa Mlandizi, Pwani ameuawa kikatili na watu wasiojulikana kisha mwili wake kutelekezwa porini.
Mwili wa mtoto Neema uliokotwa na wachunga ng’ombe katika pori la Disunyara lililopo kilometa saba kutoka nyumbani kwa akina Neema, Mlandizi Novemba mosi, mwaka huu.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, mwili huo ulikuwa umenyofolewa koromeo, meno yote ya chini na sehemu za siri huku nguo ya ndani ikiwa imewekwa pembeni.
Akizungumza kwa masikitiko na gazeti hili, baba wa mtoto huyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Nyamuhanga, alisema Novemba 27, mwaka huu, Neema alifika nyumbani akitokea shuleni kwani alikuwa anasoma darasa la awali na kutaka mama yake ampe chakula.
Baada ya kula, Neema aliondoka na hakurudi hadi usiku, jambo ambalo liliwashtua wazazi wake na majirani walioanza kumtafuta.
ALIJITABIRIA KIFO CHAKE?
Mtoto Neema alijitabiria kifo chake kwani baada ya kula chakula alimwambia mama yake kuwa amechoka na maisha anaondoka lakini mama yake alipuuzia na kuona ni maneno ya kitoto.
Cha kushangaza kweli mtoto huyo aliondoka kama vile anaenda kucheza na hakurejea tena nyumbani.
ATAFUTWA KWA SIKU SITA
Kwa mujibu wa baba Neema, walijitahidi kutoa taarifa polisi, misikitini na kumtafuta katika shule mbalimbali za Mlandizi ambapo watoto wachache walikiri kumuona akipita mitaa yao lakini hakuna aliyejua wapi mtoto huyo alipoelekea.
Kutokana na kutafuta kila sehemu bila mafanikio kwa siku sita, walitafuta njia nyingine ambapo walitumia waganga wa kienyeji kwa ajili ya kumrudisha mwanaye.
“Kweli inaniuma sana, nimepata maiti ya mwanangu, bado siamini maana nilikuwa na huyu mtoto mmoja tu na miezi michache iliyopita mke wangu alikuwa mjamzito mtoto akafia tumboni,” alisema mzazi huyo huku akifuta machozi.
USHIRIKINA WATAJWA
Katika msiba huo, wengi walikiri kuwepo kwa ushirikina kutokana na jinsi mtoto huyo alivyopotea, waganga walivyotoa vitu vya ajabu ndani ya nyumba hiyo na mtoto kutolewa baadhi ya viungo.
ALAZWA LUPANGO
Kutokana na waganga hao kuwepo nyumbani kwake, kundi kubwa la watu lilijaa na kusababisha polisi kufika eneo hilo na kumchukua baba Neema pamoja na waganga watatu ambapo alilala lupango siku mbili katika Kituo cha Polisi cha Mlandizi kwa kile kilichodaiwa kuwa hakuwa na kibali cha kujaza watu nyumbani kwake.
Baba Neema alisema uchunguzi wa daktari ulionesha kuwa mtoto wake aliuawa mbali na kutupwa eneo hilo.
Kutokana na maiti hiyo kuharibika vibaya ilipelekwa moja kwa moja nyumbani kwao na kuzikwa Novemba 2, mwaka huu katika makaburi yaliyopo maeneo hayo ya Mlandizi.
Baadhi ya majirani waliokuwa kwenye msiba huo walisema katika eneo lao hilo kumekuwa na matukio mengi ya watoto kupotea katika mazingira ya kutatanisha.
MWENYEKITI ANENA
Mwenyekiti wa Mlandizi-Kati, Ali Bakari Nyambwili alikiri kutokea kwa matukio hayo na kusema kuwa wamejiandaa kukomesha matukio hayo kwa kuanzisha ulinzi shirikishi na utambuzi kwa kila mgeni atakayeingia katika kijiji hicho.
Mwenyekiti wa Mlandizi-Kati, Ali Bakari Nyambwili alikiri kutokea kwa matukio hayo na kusema kuwa wamejiandaa kukomesha matukio hayo kwa kuanzisha ulinzi shirikishi na utambuzi kwa kila mgeni atakayeingia katika kijiji hicho.