aji wa sheria.
Chama hicho kimeeleza kusikitishwa na kitendo hicho kufanywa na Mbunge aliyehusika na upitishaji wa sheria hiyo huku wabunge wenyewe wakiwa wakali pale wananchi na wadau mbalimbali wanapohoji mapato yao.
Katibu Mkuu wa Tughe Taifa, Ally Kiwenge alisema Dar es Salaam jana kwamba pamoja na hatua hiyo kukiuka sheria ya kazi na uhusiano kazini inayosema mshahara ni siri ya mwajiri na mwajiriwa, pia kitendo hicho si ajenda ya wafanyakazi hivi sasa.
Alisema ajenda ya wafanyakazi kwa sasa ni kuona wabunge wanapigana kufa kupona katika kuhakikisha kuwa mshahara wa mfanyakazi unaongezeka kukidhi mahitaji ya mwezi mzima na kuwaondolea mzigo wa mikopo inayowaandama.
“Huu si wakati wa wafanyakazi kutaka kujua mishahara ya Rais au Waziri Mkuu, ajenda yetu kwa sasa ni kuona wabunge wanapigana ili kuboresha mishahara ya wafanyakazi ili ukidhi mahitaji muhimu tofauti na sasa,” alisema Kiwenge.
Alisema pamoja na hilo ni mkakati wa wafanyakazi sasa kuona wabunge wanatumia muda wao uliosalia kabla ya Bunge kuvunjwa kuhakikisha mambo makubwa mawili yanaingizwa katika Katiba mpya, moja ikiwa ni nafasi ya mfanyakazi kikatiba ikoje na pia kuona Katiba mpya inasema nini juu ya hatima ya maslahi ya wafanyakazi.
“Tunataka Katiba mpya itamke wazi juu ya mishahara ya wafanyakazi ili iwe ni ile inayokidhi haja,” alisema.
Aeleza kuwa ni jambo la kusikitisha kuona wabunge wanaanza kutaja mishahara ya viongozi wa taifa hadharani kwa kudhani kuwa ndio njia sahihi ya kuwasaidia Watanzania bila kujua kuwa hatua hiyo itasababisha mgawanyiko wa matabaka na kuligawa Taifa, jambo ambalo ni la hatari.
“Sisi mishahara ya viongozi wote tunaifahamu na hata ya wabunge, lakini sheria inasemaje juu ya kutangaza mshahara wa mtu hadharani? Wafanyakazi wanaweza kuitaja lakini kwa vile wameandaliwa hawafanyi hivyo, wanazingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi.
“Naamini kama wafanyakazi wangekuwa ni watu wa kukusanyana na wangekuwa hawana maadili wangeweza kusema mengi ambayo yangeshangaza jamii lakini hawafanyi mambo kwa kukurupuka au kuutafuta umaarufu usio na msingi,” alisema.
Katibu Mkuu huyo wa Tughe alisema kwa kufuata mfano wa wafanyakazi, viongozi wakiwemo wabunge watoe kauli za kujenga nchi na si zenye kuashiria matabaka na ubaguzi, jambo linaloweza kusababisha migogoro mikubwa na kuliingiza taifa katika machafuko yasiyo na tija,” alisema.
Alisema wabunge wafahamu pia kwamba suala la mishahara litaendelea kubakia kuwa ni la mwajiri na mwajiriwa na ndio maana katika fomu au nyaraka nyingine zinazoelezea majukumu ya wabunge suala la mishahara na marupurupu yao haliwekwi wazi kwa vile ni siri kati yao na taasisi ya Bunge kisheria.