Katika vurugu hizo zilizolazimisha shughuli za mahakama kusimama kwa muda wa saa mbili, askari wawili waliokuwepo eneo la tukio walishindwa kumdhibiti Manfred, kitendo kilichofanya kuitwa kwa wengine zaidi ambao waliweza kumtuliza mtuhumiwa huyo.
Hakimu Alisile Mwankejela aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo namba 322 ya mwaka 2013 pamoja na makarani wa mahakama hiyo walitimua mbio kuhofia kudhurika, mara tu baada ya vioja hivyo kuanza kufuatia kuahirishwa kwa kesi ya mtuhumiwa huyo ambayo itasomwa tena Septemba 24, mwaka huu.
“Ni kweli tukio hilo limetokea baada ya kuhairisha kesi, mshitakiwa huyo alikojoa mahakamani na kufanya vurugu kubwa,” alisema hakimu huyo alipokutwa ofisini kwake.
Karani wa makahama hiyo, Kidawa Minangu alimwambia mwandishi wetu;
“Manfed asubuhi aliletwa hapa kwa ajili ya kesi yake, alipofika tuliita jina lake na aliingia mahakamani na kusomewa mashitaka yake, kesi ilipohairishwa cha ajabu alivua suruali na kukojoa hapa mahakamani, tuliwaita askari wawili wa hapa mahakamani walipomkamata alianza kupigana nao na kuvunja meza za mahakama ndipo tulipoamua kuomba msaada wa askari wengine ambao walifika na kumdhibiti.