Dar es Salaam. Serikali imewafukuza kazi
Mkuu wa Gereza la Kiteto, Mrakibu wa Magereza, Ally Sauko na Msaidizi
wake Mrakibu Msaidizi wa Magereza Joseph Kimaro, baada ya kukamatwa na
askari wa Kikosi cha Kuzuia Ujangili Kanda ya Kati wakiwa na nyara za
Serikali.
Hivi karibuni Jeshi la Magereza lilitoa taarifa
kwamba mkuu huyo, amevuliwa uongozi na kuhamishiwa Ofisi ya Mkuu wa
Magereza wa Mkoa wa Manyara, akisubiri maamuzi ya mamlaka ya kinidhamu
wakati Kimaro alifunguliwa mashtaka na kusimamishwa kazi akisubiri
maamuzi ya mamlaka ya kinidhamu.
Maofisa hao ni miongoni mwa askari saba
waliokamatwa na kikosi hicho Julai 23 mwaka huu, wakiwa na nyara za
Serikali zenye thamani ya Sh55 milioni.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Isaac
Nantanga, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa maofisa hao
wamefukuzwa kazi kutokana na matumizi mabaya ya madaraka kwa kuruhusu
gari na silaha za Serikali kutumika katika ujangili.
“Matukio ya uhalifu kwa watendaji wa vyombo vya
dola yanaleta mshtuko mkubwa kwenye jamii na inaonekana ni suala
linaloanza kukua,”alisema Nantanga.
Alisema maofisa wengine wa ngazi za chini waliokamatwa wakiwa na nyara walishafukuzwa kazi na Kamishna wa Magereza Nchini.
Katika hatua nyingine, Msemaji huyo alisema zaidi ya wakimbizi 500,000 wamerejeshwa kwao tangu zoezi hilo lilipoanza mwaka 2002.