Akizungumza jana kwenye mkutano wa Chama cha Wabunge Wanawake
Tanzania (TWPG), kujadili mchakato wa Mabadiliko ya Katiba, Mbunge wa
Viti Maalumu (CCM), Esther Bulaya alisema wanafanya kazi nchi nzima
kuwashinda wabunge waliochaguliwa.
“Mara nyingi hawa wabunge waliochaguliwa na
wananchi wanalalamikiwa kwamba hawapatikani, lakini sisi wa viti maalumu
muda mwingi tuko na wananchi kuangalia changamoto zinazowakabili na
kuziwasilisha sehemu husika ili zitatuliwe,” alisema Bulaya. Mbunge wa
Viti Maalumu (CCM), Zarina Madabida alisema wana michango mizuri, pia
uwezo wa kuzunguka nchi nzima kutatua kero zinazowakabili wananchi.
Madabida alisema kauli ya Waziri Sitta siyo sahihi akitamba kuwa
wanafanya kazi na wakati mwingine kufika maeneo ambayo wabunge
waliochaguliwa na wananchi hawafiki.
Hata hivyo, alitaka uandaliwe utaratibu mzuri wa
kuwapata wabunge hao bila ya kujali itikadi za siasa ili
watakaochaguliwa wawe ni wachapa kazi.
Mbunge mwingine wa Viti Maalumu (CCM), Ritha
Kabati alisema hawaonekani kama wanafanya kazi kwa kuwa hawashirikishwi
kwenye Mfuko wa Jimbo jambo linalowanyima fursa ya kutoa michango yao.
Hata hivyo, Kabati alihojiwa na gazeti hili siku
chache baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutoa rasimu yake ikifuta
viti hivyo na kusema: “Ni bora Tume ya Warioba walivyoondoa viti
maalumu. Vilikuwa vinatudhalilisha, watu walikuwa hawatupi thamani
halisi kama wabunge.” Awali, akifungua mkutano huo, Spika wa Bunge,
Anne Makinda aliwataka wabunge hao kujipanga na kutokufanya makosa kufikia uamuzi kuhusu Rasimu ya Katiba.
“Hii ni fursa ya kipekee na muhimu kwenu wabunge
wanawake na Taasisi ya Bunge kwa jumla. Hatuna budi kujipanga vizuri
katika kutoa maoni yetu.
“Miaka 50 baada ya uhuru, wanawake hatuna tena
sababu na msamaha wa kutokushiriki kwenye zoezi hili muhimu
kikamilifu... wanawake tumepata uzoefu wa kutosha, tunayo elimu ya
kutosha na tunayo sauti. Kubwa zaidi ya yote tunajiamini.”
“Sisi wachache tuliokusanyika hapa tumebahatika.
Ni mithili ya taa za mbele za gari ambazo ndizo humwongoza dereva wakati
wa giza. Hivyo, tuna wajibu wa kuyasema matatizo na changamoto
zinazowakabili wanawake na makundi mengine kama vile watoto na walemavu
hususan wakati huu tunapoandika Katiba Mpya.”
“Bado kuna masuala ambayo sisi kama taasisi
tungependa yaingizwe kwenye Rasimu ya Katiba. Ni vizuri tunapoandika
Katiba Mpya, mihimili hii hususan Mahakama na Bunge iwiane ili kuleta
heshima na kuaminiana zaidi.” MWANANCHI