Home » » RAIS PAUL KAGAME HATARINI KUSHITAKIWA ICC

RAIS PAUL KAGAME HATARINI KUSHITAKIWA ICC


ONYO lililotolewa na Ikulu ya Marekani dhidi ya Serikali ya Rwanda, linalomtaka Rais wa nchi hiyo, Paul Kagame, kuacha kuwasaidia waasi wa kikundi cha M23, lina kila dalili zinazomuweka kwenye kundi la viongozi wa Kiafrika ambao hatma yao baada ya kuachia madaraka inazungukwa na wingu la mashaka.

Rais wa Marekani, Barack Obama, ambaye mapema wiki hii alikaririwa na vyombo vya habari mbalimbali duniani akimtaka Rais Kagame kuacha kukisaidia kijeshi kikundi cha waasi wa M23, anaaminika kuitoa kauli hiyo kama msimamo wa serikali yake inayopinga watawala wanaojihusisha na uhalifu wa kivita.

Ingawa hadi sasa Rais Kagame hajatajwa na Ikulu ya Marekani kama mmoja wa viongozi wa Afrika wanaotuhumiwa kwa uhalifu wa kivita, onyo lililotolewa na Rais Obama linadhihirisha kuwepo kwa ushahidi unaomhusisha na matukio ya aina hiyo yaliyopata kuwagharimu baadhi ya marais walionyooshewa kidole na Marekani kwa aina hii hii anayonyooshewa sasa Kagame.

Wadadisi na wafuatiliaji wa mambo walioichambua kauli ya Rais Obama, wanaeleza kuwa aliitoa baada ya Marekani kujiridhisha na ushahidi ilioukusanya ukiihusisha Serikali ya Rwanda kuwasaidia waasi wa kundi la M23.

Wanaeleza kuwa Marekani baada ya kubaini ushirika wa majeshi ya Rwanda yaliyojipenyeza ndani ya makundi ya waasi wanaopigana na Serikali ya Kongo, huku wakitekeleza vitendo vya kinyama dhidi ya binadamu katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa madini, imeamua kumtosa Kagame, ambaye amekuwa na uswahiba wa muda mrefu na taifa hilo.

Katika tathimini yao kuhusu uzito wa onyo la Rais Obama kwa Rais Kagame, wanaeleza kuwa hataweza kuepuka kitanzi cha mashitaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC).


Waasi wa kikundi cha M23, mbali na kuendesha mapambano dhidi ya majeshi ya Serikali ya Kongo, jambo linalopingwa na jumuiya ya kimataifa, pia wanatuhumiwa kwa ubakaji na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.

Tuhuma hizo pia zinaelekezwa kwa majeshi ya Rwanda, yanayodaiwa kushirikiana na waasi hao na ndizo zinazomuweka Rais Kagame katika hatari ya kufikishwa mahakamani na hata kuhukumiwa kama ilivyokuwa kwa aliyekuwa Rais wa Liberia, Charles Taylor, ambaye kwa sasa anatumikia kifungo cha miaka 50 jela baada ya kupatikana na makosa ya uhalifu wa kivita nchini Sierra Leone ambako zaidi ya watu 50,000 waliuawa katika vita ya wenyewe kwa wenyewe na wengine wengi wakiachwa na ulemavu wa kudumu.

Kama inavyotokea kwa Rais Kagame sasa, kwa Taylor pia ilikuwa hivyo hivyo, pale alipokuwa akionywa na jumuiya za kimataifa na yeye kudharau maonyo hayo.

Wakati wadadisi na wachambuzi wa mambo wakiwa na mtizamo huo kuhusu onyo la Serikali ya Marekani dhidi ya Rais Kagame kujiingiza kijeshi katika vita vya ndani ya Kongo, ushahidi uliokusanywa na taasisi za Umoja ya Mataifa za kutoa misaada ya kibinadamu unaonyesha kuwa wanajeshi wa Rwanda wanaopigana bega kwa bega na waasi wa M23 wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya kihalifu dhidi ya binadamu.

Ni ushahidi wa aina hiyo ndio uliotumiwa na ICC, kumhukumu Taylor, aliyekuwa akituhumiwa kuvisaidia vikundi vya waasi vya Revolutionary United Front (RUF) na Armed Forces Revolutionary Council (AFRC) kwa kuvigawia silaha za kivita kwa muktadha wa kupewa madini ya almasi.

Stephen Rapp, mchambuzi wa sheria za makosa ya jinai wa Marekani, katika mahojiano yake na gazeti la The Guardian la nchini Uingereza, alieleza kuwa uongozi wa Serikali ya Rwanda una tuhuma za kujibu katika Mahakama ya ICC, kuhusu mapigano yanayoendelea Mashariki mwa Kongo.

Kauli hiyo ya Rapp inaunga mkono madai ya mara kwa mara ya mashirika ya kimataifa yanayojihusisha na utetezi wa haki za binadamu ya Human Right Watch, Save the Children, UNICEF na UNHCR, ambayo kwa nyakati tofauti yamekuwa yakidai kuwa na ushahidi wa kutosha wa waasi wa M23 kusaidiwa na Jeshi la Rwanda kufanya mauaji ya raia wasiokuwa na hatia katika miji mbalimbali ya Mashariki mwa Kongo.

Inadaiwa pia kuwa upo ushahidi unaoonyesha jinsi ambavyo waasi wa M23 wamekuwa wakiwatumia watoto wadogo katika vikosi vya majeshi na ndio ambao wamekuwa wakitangulizwa mstari wa mbele katika uwanja wa mapambano, hususan katika matukio ya uhalifu wa kivita.

Tuhuma nyingine zinazoelekezewa Serikali ya Kigali ni kufadhili kundi la waasi la CNDP, lililokuwa chini ya uongozi wa Jenerali Bosco Ntaganda, ambaye amejisalimisha kwenye Mahakama ya ICC mapema mwaka huu.

Sehemu kubwa ya wapiganaji wa kundi la Ntaganda sasa wameungana na waasi wa kundi la M23 na wamekuwa wakijiimarisha kiulinzi katika maeneo yenye utajiri mkubwa wa madini nchini Kongo.

TOA MAONI YAKO HAPA

 
Support : Copyright © 2011. HABARILINE - All Rights Reserved